Mgogoro wa ardhi kati ya mwekezaji wa shamba la malonze na Wananchi wa Vijiji vinavyozunguka shamba hilo umechukua sura mpya baada ya Wananchi kulalamika maeneo ya vijiji vyao kutwaliwa hivyo kukosa ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Wakati wao wakitoa madai hayo, Mwekezaji naye amewalalamikia Wananchi hao kuingilia mipaka ya shamba lake alilouziwa na Serikali.
Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa kamati Maalum ya Bunge ya kuchunguza Mgogoro huo, Prof. Shukrani Manya wakati akisoma taarifa ya sakata hilo jijiji Dodoma.
Amesema, “nyaraka muhimu na matokeo ya mahojiano kwa pamoja vinaonesha kwamba, tangu enzi za Bi Isle Damm, wananchi walikuwa wakitumia sehemu ya shamba hilo kwa makazi, kilimo na ufugaji.”
Prof. Manya ameongeza kuwa, “mwaka 1977, Serikali iliunda Kamati ndogo ya Wilaya iliyopendekeza kuwa NARCO ipunguze ekari 10,007 na zigawiwe kwa baadhi ya vijiji vinavyozunguka shamba hilo, jambo ambalo liliridhiwa na NARCO.”
Amesema, kwa hatua za Serikali za kuelemisha wananchi kutofanikiwa kuzuia mgogoro ni ishara kwamba, hazikuwa na uhalisia au hazikugusa kiini cha msingi cha tatizo Hivyo, kufanya mgogoro kuendelea kuwepo.
Hata hivyo Prof. Manya amedai tathmini inaoenesha kwamba, Mwekezaji anatafsiri mwingiliano huo wa mipaka sawa na tafsiri iliyotolewa na Waziri na Kamishna wa Ardhi.
“Pamoja na hivyo, ni ukweli kwamba, wananchi wa vijiji vinavyozunguka shamba vikiwemo vijiji vya Sikaungu, Songambele Azimio na Msandamuungano kwa muda mrefu wanatambua mipaka ya vijiji vyao kwa kutumia alama za asili kama vile mito ambayo ipo kwenye ramani zilizosajiliwa mwaka 2009,” alifafanua.
“Kwa msingi huo, wameendelea kuamini na kutambua kuwa sehemu ya shamba iliyo ndani ya mipaka ya kijiji ni ardhi ya vijiji vyao,” amesema.