Lydia Mollel – Morogoro.

Kuchimbwa kwa Kisima cha kudumu cha maji kwa Shule ya Msingi Mazimbu A na B, kunatazamiwa kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi ambapo awali yalikuwa ya kusuasua kufuatia ukosefu wa maji safi na salama uliogubika shule hizo kwa muda mrefu.

Hayo yamebainishwa na Miriam Bosco ambaye ni Mwanafunzi wa Darasa la sita katika shule ya Msingi Mazimbu B, wakati akielezea changamoto ya ukosefu wa maji ulivyoathiri baadhi yao kushindwa kuhudhuria masomo, kwa kuhofia kuhatarisha afya zao kwa uchafu wa vyoo uliokithiri.

Amesema, kukosekana kwa maji kumechangia mazingira ya shule kutoonekana nadhifu, mimea ikishindwa kustawi licha ya wanafunzi kwenda shuleni na maji ya kumwagilia mimea pamoja na kufanyia usafi wa vyoo, bado vinyesi vilionekana juu ya matundu ya vyoo.

“Mazingira ya usafi shuleni yalikuwa ni machafu sana kwa kukosa maji shuleni lakini pia tulikuwa tunashindwa kumwagilia mimea na Wanafunzi wanakosa maji ya kunywa, tunlazimika kuja na maji kutoka nyumbani muda mwingine tunasahau, tukija shule hakuna maji siku nyingine yanotoka kidogo, madarasa hayadekiwi, na hata vyoo vipo katika hali mbaya, unakuta muda mwingine vinyesi vimejaa tunashindwa kuvitumia, hii imeathiri sana mahudhurio ya wanafunzi hususani wanafunzi wakike,” alisema Miriam.

Naye Junior Omary, Mwanafunzi wa Shule Mazibu B  amesema kuchimbwa kwa kisima kutaleta afuu shuleni hapo, wanafunzi walikosa shuleni hasa mabinti waliokwisha pevuka kwa kuwa mazingira ya vyoo hayakuwa salama kwao.

“Hapa shuleni wanafunzi wakike waliokwisha kupevuka wanashindwa kuhudhuria masomo na muda mwingine wanatoroka shule kwasababu shuleni hakuna maji na mazingira ya vyoo sio salama kwao, hivyo wanaona bora wabaki nyumbani kuliko kuja shule kuteseka, uchafuu wa vyoo ungeweza kutusababishia magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu na magonjwa ya kuhara” Alisema Omary.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu Shule ya Mazimbu A, Asteria Paulo,amesema ukosefu wa maji umekuwa ukileta usumbufu mkubwa katika kuendesha vipindi vyao vya masomo, maji ya MORUWASA waliyokuwa wakitumia walikuwa wakilipa bili kubwa licha ya kupata huduma hiyo mara moja moja

“Kiukweli tunamshukuru Mungu amekuwa akitulinda na kutuepusha na magonjwa ya mlipuko, tumekuwa na maji ya MORUWASA hapa malipo ni makubwa kulingana na wingi wa wanafunzi na wamekuwa wakitutishia kukata, lakini pia changamoto ya maji imekuwa ikisababisha utoro wa wanafunzi na kuwafanya baadhi yao kushindwa kufanya vizuri shuleni lakini kwa sasa tumepata maji mengi mazingira yatakuwa masafi” Alisema Paulo.

Katika hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kiraia la Educational Gauge for Growth Tanzania (EGG), Jumanne Mpinga amesema wameshirikiana na Ofisi ya Balozi wa Uturuki kuchimba visima viwili vilivyogarimu milioni 28 kws Manispaa ya Morogoro ambavyo vitaleta mabadiliko makubwa, si tu katika shule hizo bali pia katika jamii zinazozunguka.

“Kwa mara nyingine tena tumefanikisha miradi miwili katika Manispaa ya Morogoro, moja ni katika shule ya Msingi Mazibu A na B, Pili ni kisima kimoja katika shule ya Sekondari Tungi estate, visima hivi jumla vimegarimu takribani millioni 28, kimsingi ni kajili ya kuwahudumia wanafunzi na jamii zinazowazunguka” Alisema Mpinga.

Aidha Balozi wa Uturuki Tanzania Mehmet Gulluoglu, amesema wataendelea kudumisha  uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Uturuki kwani miradi mbalimbali itaendelea kufanyika ili kuboresha hali ya uchumi ulipo kwa sasa.

Kisa Bahati Nasibu: Ajenga Nyumba mbili kwa mpigo
Ukurugenzi WHO: Ndugulile aiheshimisha Tanzania