Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Norman Jonas amesema mpango mkakati wa Afya na lishe shuleni una mchango mkubwa katika kuimarisha Afya na ufaulu kwa Wanafunzi.
Dkt. Norman ameyabainishwa Mkoani Morogoro katika ufunguzi wa Kikao kazi cha kuandaa Mpango Mkakati wa Afua za Afya na lishe shuleni kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Amesema, lengo la Mpango mkakati huo ambao ni wa miaka mitano inayokuja ni kuboresha afya za wanafunzi kuanzia shuleni hadi vyuoni na kwamba miongoni mwa mambo muhimu katika mkakati huo ni pamoja na kuboresha afya, elimu kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza, umuhimu wa kufanya mazoezi.
Kwa upande wake, Mratibu wa Mpango wa Taifa wa Afya Shuleni kutoka Wizara ya Afya, Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma Beauty Mwambebule amesema kupitia Mpango Mkakati huo pia watazungumzia juu ya suala umuhimu wa mlo sahihi shuleni pamoja na namna gani ya kujiepusha wanafunzi kujiepusha katika makundi hatarishi.
“Tunaangazia suala la mlo shuleni mfano watoto wanakula vitu vya sukari muda wote hali ambayo hupelekea magonjwa yasiyoambukiza, presha ,na tunaangazia namna gani watoto shuleni wanaweza kujiepusha katika vitendo hatarishi mfano ngono katika umri mdogo hivyo kupitia Mpango mkakati utawezesha namna ya kuongea na mtoto shuleni”amesema .
Kwa upande wake Mratibu wa Programu ya Elimu ya Afya na Ustawi kutoka UNESCO Mathias Faustine amesema katika kuhakikisha ubora wa elimu kwa watoto na vijana shuleni lazima pawe na lishe bora.
“Tunashukuru serikali kwa kuwa mstari wa mbele katika utengenezaji wa Mpango Mkakati huu wa miaka mitano ambapo mtoto ili afanye vizuri lazima awe na afya na lishe na mpango huu utakuwa dira pia utasaidia kila mtoto na kijana shuleni kujikinga na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo UKIMWI.” amesema.
Kikao kazi cha kuandaa Mpango Mkakati wa Afua za Afya na lishe shuleni kinafanyika kwa siku tano mkoani Morogoro kuanzia tarehe 27 hadi,31, Agosti, 2024 ambapo Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na wadau ikiwemo UNESCO, UNFPA na wadau wengine wanajadili namna bora ya kuimarisha Mpango mkakati wa Afya na lishe shuleni.