Shirika la Reli Tanzania – TRC limeutaarifu umma kuwa treni ya abiria namba Y14 ikiwa nakichwa cha treni namba 9002, mabehewa 12 ya abiria, behewa moja la vifurushi na behewa moja la breki imepata ajali kati ya Stesheni ya Kazuramimba na Uvinza mkoani Kigoma.
Tarifa ya TRC iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano, Jamila Mbarouk imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea majira ya Saa 7.30 usiku Agosti 28, 2024 baada ya mabehewa sita ya treni kuacha njia na kupelekea majeruhi 70, Wanawake 26 na wanaume 44.
Treni hiyo ilikuwa na jumla ya abiria 571 wakisafiri kutoka Kigoma kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam ambapo TRC kwa kushirikiana na Kitengo cha Afya cha Mkoa wa Kigoma walifanikiwa kuwapeleka majeruhi katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza kwa ajili ya matibabu.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, hali za afya za abiria zinaendelea kuimarika ambapo majeruhi 57 tayari wameruhusiwa, nane wanaendelea na matibabu katika hospitali ya Wilaya ya Uvinza na watano wamehamishiwa Hospitali ya Maweni kwaajili ya matibabu zaidi.
Hata hivyo, Treni iliendelea na safari kuelekea mikoa ya Tabora, Dodoma, Morogoro,Pwani na Dar es Salaam ambapo TRC imesema inawapa pole majeruhi na inaendelea na jitihada za kuwahudumia huku kukiwa hakuna taarifa yavifo vilivyotokana na ajali hiyo na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.