Kamati ya Kudumu ya Bunge ya miundombinu imebaini kwamba, pamoja na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania kupitia Tangazo la Serikali Na. 404 la mwaka 1999 Mamlaka iliyopo sasa imekuwa ikitekeleza majukumu yake kama Wakala chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali, Sura ya 245, na kusimamiwa na Bodi ya Ushauri ambayo ina mamlaka finyu.
Ameyasema hayo Mwenyekiti wa kamati Moshi Kakoso, wakati akisoma maoni ya kamati ya kudumu ya Bunge kuhusu muswada wa sheria ya Viwanja vya ndege Tanzania ya Mwaka 2025 ambapo amesema baadhi ya viwanja vya ndege vya Serikali viliendelea kusimamiwa na kuendeshwa na taasisi nyingine za Serikali hali ambayo ilisababisha kutowekupo kwa mfanano katika usimamizi na uendeshaji wa jumla wa viwanja vya ndege vinavyomilikiwa na Serikali.
“Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Sheria inayopendekezwa kutungwa na Muswada inapendekeza kuipatia Mamlaka ya Viwanja Ndege (TAA) mamlaka kamili kisheria ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi chini ya Bodi ya Utendaji ambayo Mwenyekiti wake atateuliwa na Rais,” amesema.
“Sheria inayopendekezwa, iwapo itasimamia vizuri, itaiwezesha Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kuongeza ufanisi wake na hatimaye kuongeza ubora wa huduma zitolewazo katika viwanja vya ndege vya Serikali,” amesema Kasoko.
Amesema kwa muktadha huo, na kwa kuzingatia ukweli kwamba viwanja vya ndege ni lango la kiuchumi, kiutalii na kimaendeleo, Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha kwamba, Viwanja vya Ndege vya Serikali nchini vinakidhi vigezo vya ICAO katika ubora wa miundombinu na huduma za msingi.
Ameongeza kuwa, “pia Kamati iliishauri Serikali ipasavyo kuhusu umuhimu wa kubakiza fedha zitokanazo na tozo ya huduma kwa abiria (retention of passengers’ service charge) kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).”
“Kamati ilishauri Serikali kuwasilisha marekebisho ya sheria yatakayoweka utaratibu wa kubakiza kwa TAA fedha zitokanazo na tozo hiyo ili kuipunguzia taasisi hiyo utegemezi wake kwa Serikali Kuu na kuiwezesha kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege nchini,” amesema Kasoko
Aidha ameongezea kwa kusema Kamati ya Bajeti iliitaka Serikali kuwasilisha fedha zote zinazokusanywa na zitakazokusanywa katika mwaka wa fedha 2024/2025 kutoka kwenye chanzo hiki kwa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege.