Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro Agosti 30, 2024 akiwa Mkoani Manyara ametembelea na kukagua eneo la ujenzi wa kituo cha umahiri katika michezo mbalimbali hususani mchezo wa riadha kwa kanda ya kaskazini.
Akizungumza katika ziara hiyo amesema lengo la serikali ni kuinua michezo nchini ili kuongeza ushindani katika mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Olimpiki na Jumuiya ya Madola.
“Lengo la serikali ni kufungua vituo hivi katika kanda zote nchini, kila kituo kitakuwa na umahiri wake, hiki kitakua mahiri katika riadha, hivyo tumekuja kutekeleza sera ya michezo na ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi kwa kuhakikisha michezo inakua ajira na uchumi kwa kuwaandaa vijana” Amesema, Ndumbaro.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha amesema, ujenzi huo, utaanza kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2024/2025 ambapo tayari fedha imesha tengwa na mchakato wa kumpata mshauri elekezi upo katika hatua za mwisho.
Naye Mbunge wa Jimbo la Babati Mjini, Pauline Gekul ameishukuru Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao utasaidia kuibua na kukuza vipaji ambavyo vipo katika katika eneo hilo.