Katibu Tawala wa Wilaya ya Mvomero, Said Nguya amewasisitiza wazazi kuwa hakuna akili za Kurithi kwa mtoto, kwani uwezo wa akili wa mtoto hutokana na lishe bora anayoipata mtoto tangu siku ya kwanza mwanamke anapopata ujauzito.
Nguya ameyasema hayo, alipokuwa akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi katika mahafali ya Shule ya msingi KwaMuhuzi iliyopo Dakawa wilayani Mvomero.
Katibu Tawala amekemea pia tabia ya baadhi ya wazazi kutowahimiza watoto wao suala la mahudhurio ya shuleni, badala yake kuwatumia kwenye mashamba ya Mpunga kama nguvu Kazi, jambo ambalo limefanya utoro kuzidi kuota mizizi na baadhi yao kuacha kabisa masomo.
Nguya ameeleza kuwa, kama wazazi wasipowaandaa vijana wao sawasawa, kimaadili na kiakili, miradi mikubwa inayotekelezwa na Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, itaendeshwa na watu kutoka maeneo mengine badala ya wao kuwa sehemu ya kuiendesha miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa wazazi kuwaandaa vema vijana wao.