Serikali imesema inaendelea na utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kupitia bajeti ya 2024/2025 jumla ya miradi 1,095 inatarajiwa kutekelezwa vijijini na miradi 247 mijini.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Mathew leo Septemba 2, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa jimbo la Arumeru Magharibi Noah Saputu aliyeuliza Serikali ina mkakati gani mahsusi wa kukamilisha miradi ya maji mikubwa na midogo nchini.

Mhandisi Kundo amesema Miradi hiyo inatekelezwa ili kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 85 vijijini na 95 mijini ifikapo mwaka 2025/26.

“Mheshimiwa Spika; nia ya Serikali ni kuhakisha miradi ya maji yote mikubwa na midogo iliyopangwa kutekelezwa na inayoendelea na utekelezaji nchini inakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma iliyokusudiwa kwa wananchi”

“Mkakati mahususi wa Serikali ni kuhakikisha inepeleka fedha zinazohitajika kwenye utekelezaji wa miradi hiyo kwa wakati sanjari na kusimamia utekelezaji wake” amesema Mhandisi Kundo.

Mpya: Uteuzi, uhamisho wa Viongozi mbalimbali
Wazazi hakuna akili za kurithi - DAS Nguya