Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema mageuzi ya kiuchumi ya Indonesia katika sekta mbalimbali kama vile uchimbaji wa mafuta na gesi, kilimo na viwanda vimeiwezesha nchi hiyo kuwa nafasi ya 10 kiuchumi duniani.
Mafanikio hayo yameihamasisha Tanzania kujifunza kutoka nchi hiyo, hasa kwa kuzingatia walivyoweka vipaumbele vya utekelezaji wa sera za kiuchumi zinazolenga ustawi wa wananchi na ukuaji wa taifa kwa ujumla.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Indonesia na Afrika 2024, ambao umefunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Joko Widodo, uliofanyika katika ukumbi wa mikutano, hoteli ya Mulia, Bali, Indonesia.
Dk. Mwinyi katika jukwaa hilo amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema, Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo sekta ya uchumi wa buluu ambapo ndani yake kuna kilimo cha mwani, miundombinu ya bandari, ufugaji wa samaki, pamoja na uvuvi wa bahari kuu, eneo ambalo lina hazina kubwa ya samaki na soko hilo bado halijafanyiwa kazi ipasavyo.
Zanzibar imepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya samaki waliovuliwa kutoka tani 38,107 mwaka 2020 hadi tani 80,000 kufikia Desemba 2023.
Wakati huohuo, Rais Dkt. Mwinyi alipata fursa ya kuzungumza na viongozi wa juu wa Serikali ya Indonesia, akiwemo Rais wa nchi hiyo, Mhe. Joko Widodo, ambapo alionesha utayari wa kuhimiza makampuni na mashirika ambayo yapo chini ya Serikali ya Indonesia kuja kuangalia fursa za uwekezaji Tanzania.
Naye Waziri wa Utalii wa Indonesia, Sandiaga Uno, amemuahidi Rais Dk. Mwinyi kutoa fursa kwa vijana wa Kizanzibari kwenda nchini Indonesia kujifunza na kujenga ujuzi katika sekta ya utalii.