Kama hujatembelea kurasa ya Mabalozi wa Usalama Barabarani – RSA, basi leo Septemba 3, 2024 Admin ameelimisha kuhusu watu kujiuliza, iwapo unapopanda basi ni zipi sehemu salama zaidi kwako kukaa, kati ya siti za mbele, siti za katikati na siti za nyuma.
Anasema kwa jinsi muundo wa basi ulivyo, siti salama kuliko nyingine ni zile za katikati ya basi. Ni mara chache sana inatokea gari likapata ajali ya kugongwa katikati.
Ajali nyingi zinahusisha gari kugongwa kwa upande wa nyuma (rear-end collision) au kwa mbele (head on). Na siti zilizo salama kabisa ni zile zilizo kwenye safu kati ya tairi na tairi.
Ukiacha uimara katika ujenzi wa bodi za mabasi, kisayansi unapotokea mgongano (colission), nishati mwendo (kinetic energy) inayotengenezwa kwenye mgongano huo husafiri toka Point of impact hadi mwishoni mwa chombo husika.
Nishati hiyo, ndiyo inayoua au kujeruhi kwa sababu ni kubwa mno kwa binadamu kuivumilia. Sasa nishati hiyo ikiwa safarini hadi inafika katikati ya basi inakuwa imepunguza nguvu.
Teknolojia za kisasa za kuzuia madhara ya ajali, zimeanza kuendelezwa kwa kuweka vifaa mbalimbali vyenye kusaidia kupunguza nguvu ya nishati mwendo wakati wa ajali.
Baadhi ya vifaa hivyo ni puto za hewa (air bags) na upande wa mbele wa gari kunawekwa nafasi wazi ya nyongeza kwa lengo la kunyonya nguvu ya nishati mwendo. Sehemu hiyo huitwa Crample zone au crash zone.
Ni sehemu inayotakiwa kuchakaa ikigongwa, ili nishati mwendo iishie pale isiwafikie abiria. Iwapo sehemu hiyo itafanywa imara sana, itakapotokea ajali chuma husika hakitapinda wala kuchakaa nishati mwendo itasafiri moja kwa moja hadi kwa abiria bila kupunguzwa nguvu na kujeruhi au kuua.
Hii ndio sababu zile bus za zamani aka sufuria zikipata ajali zimekuwa zikichinja sana kuliko bus za kisasa zenye matirio ya fiber na vyuma imara kwenye mihimili au fremu ya basi.
Unatakiwa kufahamu kuwa, ikitokea ajali kama gari lilikuwa linaenda kwa mwendo wa 80Kph basi viungo vyako vya ndani navyo vitakuwa vinasafiri kwa spidi hiyo hiyo ndio maana mtu anakufa.
Sasa kupunguza spidi hiyo, sehemu ya mbele na nyuma ya gari inawekwa materia laini ili kusaidia kupunguza mwendo.
Admin amemalizia kwa kusema imani yake kuwa umeelewa na usipende kugombania sana siti za mbele.