Kampeni ya Nishati Safi ya kupikia, imeungwa mkono na Ubelgiji ambayo imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo ya Bara zima la Afrika iliyoasisiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Naibu Waziri wa Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameyabainisha hayo katika kikao chake na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van Der Straeten kilichofanyika mjini Windhoek, Namibia ikiwa ni sehemu Mkutano wa Nchi za Afika kujadili matumizi Hydrojen kutumika katika kuzalisha umeme.
Amesema, ili kupata maendeleo ya kweli, Tanzania inatoa kipaumbele katika matumizi ya nishati ambayo itawawezesha kupata maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja kuondokana na magojwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi.
“ Kama mnavyofahamu, Tanzania kupitia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeasisi na inaendeleza kampeni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka huu,” amesema Dkt. Biteko.
Kwa upande wake, Waziri Tinne amesema nchi yake iko tayari kuunga mkono jitihada za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni mkakati wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kukuza pato na maendeleo ya kiuchumi na kwamba matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati safi ni njia mojawapo ya kuchochea maendeleo ya watu na uchumi wa nchi husika.
Mkutano wa Hydrojen unaoendelea nchini Namibia unalenga kuibua fursa na changamoto zilizopo katika matumizi ya nishati hiyo, ambapo Tanzania itapata fursa ya kujifunza kuhusu matumzi ya Hydrojeni kuzalisha umeme ukihuhudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi za Afrika unatarajiwa kuhitimishwa Septemba 5, 2024.