Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema ndoto za Wanamajumui wa Afrika (Pan Africanism) zimeanza kuthibitishwa kwa Waafrika wenyewe kuwekeza katika mipango ya maendeleo ya muda mrefu ikiwemo ya elimu, afya, kilimo, uvuvi na madini.
Ushirikiano baina ya nchi za kiafrika katika sekta mbalimbali utaziwezesha kuondokana na minyororo ya kikoloni kama ilivyokuwa katika malengo ya waasisi wa nchi hizo, Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Septemba 4, 2024 wakati alipotembelea Chuo cha Triumphant kilichopo Windhoek, Namibia ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Kimataifa wa Hydrogen Barani Africa (Global African Hydrogen Summit).
Akitoa mfano wa ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Namibia amesema Chuo cha Triumphant hivi karibuni kitakuja na mpango wa mafunzo ya Lugha ya Kiswahili ambapo Tanzania kupitia Chuo Kikuu Huria kitatoa walimu wa Lugha hiyo.
Akiwa Chuoni hapo, Dkt. Biteko ameambatana na Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Caesar Chacha Waitara, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesemi Mramba, Kamishna wa Nishati, Mha. Innocent Luoga pamoja na Maafisa mbalimbali kutoka ubalozini ambao wameshuhudia maabara mbalimbali ikiwemo chumba cha kompyuta.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chuo hicho, Prof. Geoffrey Kiangi amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri Wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwa kutenga muda wake na kufanya ziara chuoni hapo.