Serikali Nchini, imesema itaendelea kujiimarisha kidiplomasia na itaongeza nguvu zaidi ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata fursa mbalimbali katika jumuia za kimataifa.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokutana na Mkurugenzi Mkuu Mteule wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika (WHO) Dkt Faustine Ndungulie, Ofisini kwake Mlimwa Jijini Dodoma na kudai kuwa pia imefanikisha kuimarisha ushirikiano baina ya nchi washirika na sasa mafanikio yanaonekana.
Amesema, “Rais wetu ameonesha nia njema katika kipindi chake cha miaka mitatu na nusu amefanya kazi kubwa ya kujenga diplomasia na mahusiano katika sekta mbalimbali na nchi nyingi duniani.”
Majaliwa ameongeza kuwa, jitihada hizo za Serikali ya awamu ya sita zimeiwezesha Tanzania kuendelea kupaa kidiplomasia kuiwezesha nchi kupata viongozi wakubwa ndani ya Taasisi za kimataifa.
“Tunaamini kazi kubwa tulizozifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kumpata spika wa Umoja wa Mabunge duniani haikuwa kazi ndogo, na tena tumepata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika,” alisema Waziri Mkuu.
Kwa upande wake Mkurugenzi huyo Mtarajiwa wa Shirika la Afya Duniani Kanda ya Afrika DKT. Faustine Ndungulile amemshukiru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuunga mkono na kufanya ushawishi wa kidiplomasia ili kufanikisha ushindi huo.
“Kwa upekee sana ninamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa katika kufanikisha ushindi huu kwa ushawishi wake kwenye jumuia za kimataifa pia nawashukuru viongozi wengine wa Serikali, Bunge na wadau wote,” alisema.