Wamiliki wa viwanda nchini, wametakiwa kuweka mifumo ya majitaka kuepusha yasitiririke ovyo na kuchafua mazingira na kuathiri afya za wananchi ikiwemo kuelimisha namna bora ya kufuata sheria ya mazingira na kuongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua uzingatiaji wa sheria ya mazingira katika kiwanda cha kurejeleza taka za mifuko chakavu na za plastiki kwa ajili ya kuzalisha viatu, mabomba na mifuko cha Future Colorful kilichopo jijini Dodoma alipfanya ziara ya kukagua uzingatiaji wa sheria ya mazingira.
Amesema, wenye viwanda wanapaswa kutafuta njia bora ya kuyarejeleza, ili yatumike tena katika shughuli za viwanda, hatua itakayowapunguzia pia gharama ya matumizi ya maji hayo huku akibaini shehena ya taka ambazo zinatumika kama malighafi ikiwa imekusanywa bila kufunikwa hivyo alielekeza uongozi wa kiwanda hicho kuihifadhi vizuri kwa kuhakikisha inafunikwa.
“Tunawapongeza sana kwa kukusanya taka hizi na kuzirejeleza lakini changamoto tuliyoiona hapa ni hizi taka kuwa wazi hivyo, ni muhimu kuandaa mazingira mazuri ya kuzihifadhi, mvua ikinyesha zinakuwa taka na sio malighafi tena ipigwe sakafu mfuniko wa kufunika malighafi hizi,“ alisisitiza Dkt. Kijaji.
Aidha, amewataka wawekezaji wa viwanda kuwaajiri wataalamu wa mazingira watakaofanya kazi nao kuhakikisha masuala muhimu na maelekezo kuhusu utunzaji wa mazingira yanafuatwa.