Wakuu wa Idara, Watumishi wa Afya, Watendaji Kata na Vijiji pamoja na Maafisa Tarafa Wilayani Mkalama, wametakiwa  kutoa elimu kwa wananchi namna ya kujilinda na ugonjwa wa homa ya Nyani maarufu kama Mpox.
Wito huo, umetolewa hii leo Septemba 5, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Moses Machali wakati wa kikao cha afya ya Msingi wilayani Mkalama kilichofanyika kwenye ukumbi ulipo ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mkalama.
Amesema, “Wakuu wa Idara, watumishi wa afya, Watendaji kata na Vijiji pamoja na Maafisa Tarafa kwa pamoja twendeni tukaelimishe jamii kuhusu homa ya nyani na namna ya kujilinda na ugonjwa huu.”
Aidha katika kuhakikisha wananchi wanajilinda na ugonjwa huo, Machali amepiga marufuku wananchi kusalimiana kwa kupeana mikono, ili kujilinda na ugonjwa huo na kutoa agizo kuwekwa maji yanayotiririka pamoja na sabuni katika maeneo yote ya taasisi za umma pamoja na yale yenye watu wengi.
Awali, akiwasilisha hali ya ugonjwa huo, Afisa Afya Wilaya ya Mkalama, Dorice Damiani amesema kuwa ugonjwa huo unaambukizwa kwa njia mbalimbali ikiwemo kushikana mikono, kujamiana na mtu mwenye ugonjwa huo pamoja na kuchangiana nguo.

Ruvu: Wahitimu JKT waahidi kulinda rasilimali za Taifa
Jifunze kwa Tai: Jambo jema haliji kirahisi