Heldina Mwingira, Dar24 Media – Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamusi, neno ukatili ni hali ya kusababisha kwa makusudi mateso na kukosesha raha dhidi ya mtu mwingine, ilihali suluhisho la wazi linaweza kupatikana kwa urahisi, na unaweza kugawanyika katika namna mbalimbali ambazo zitatafsirika kwa maana moja.
Ukatili unaweza kutokana na matatizo ya kisaikolojia yenye mizizi utotoni, lakini pia ni tabia ambayo mtu anaweza kujijengea kinyume cha maadili na mara nyingi neno hili hutumika katika sheria kuhusu matendo hasi dhidi ya watoto, wenzi wa ndoa, wafungwa na hata wanyama.
Kwa sasa dunia imekumbwa na ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni, kama ambavyo tumeona hapo juu kuwa unaweza ukatokea kwa namna nyingi, ikiwemo kutumia picha za utupu au video za utupu kama kulipiza kisasi na kutumia maneno yasiyo na staha yaani matusi na kejeli kwa jinsia ya kike kwa kujua aama kwa kutokujua na Tanzania pia imeathiriwa kiasi sasa wameibuka Wanaharakati, Taaasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali katika kuangazia ukubwa na suluhu ya changamoto hiyo.
Wahusika ambao wanafanya ukatili huo, wanaweza kuwa wenza wa sasa au wa zamani, watu wanaofanya kazi pamoja, waliosoma katika shule moja, ndugu, marafiki na watu binafsi na kutokana na ukatili dhidi ya Wanawake mtandaoni, Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali zimekuwa zikiwasaidia waathiriwa kisheria, kijamii na elimu kwa jamii.
Muathirika wa ukatili wa namna hii anaweza akawa mtu yeyote bila kujali umaarufu, cheo au hali ya kichumi
Hatua zinachukuliwa Kimataifa
Hivi karibuni zaidi ya Wanawake 200 wa hadhi ya juu, wametia saini barua ya wazi kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya unyanyasaji, iliyotiwa saini na Wanawake hao akiwemo Waziri Mkuu wa zamani wa Australia, Julia Gillard, Mchezaji wa zamani wa Tennis wa Marekani, Billie Jean King, Muigizaji wa filamu wa Uingereza, Thandiwe Newton na Emma Watson – na imechapishwa katika Baraza la Usawa la Kizazi cha UN.
Barua hiyo inasema: “kiwango cha ukatili dhidi ya wanawake mitandaoni kuongezeka kinaashiria, ulimwengu wa kidijitali sio salama. hali hii ni tishio kwa upatikanaji wa usawa wa kijinsia,” ikielekezwa kwa Maafisa wakuu watendaji wa mitandao ya kijamii ya Facebook, Google, TikTok na Twitter, kuwataka “wapatie kipaumbele usalama wa wanawake katika mitandao.
Hali hiyo ilipelekea Viongozi hao na watendaji wa mitandao ya kijamii kuahidi uimarishaji wa mifumo ya kuripoti ukatili, japo wanaharakati wameonekana kupata hofu katika suala la utekelezaji wa ahadi hiyo.
Elimu zaidi.
Kwa kuona changamoto hii imezidi kupamba moto DW akademie wamejikita na vyombo vya habari, ili kuweza kusaidia kunusuru Wanawake katika kufanyiwa ukatili Mtandaoni na imeamua kusisitiza kwa kutoa kwa mafunzo kwa baadhi ya vyombo vya habari kuhusu namna gani ya kuripoti kesi za ukatili mtandaoni.
Lengo ni kuona vyombo vya habari vinakuwa si sehemu ya kufanya ukatili mtandaoni kwa kuacha kuripoti tukio na kutakiwa kufuata Iceberg model wakati habari inaporipotiwa. Dar24 imekuwa sehemu ya wanufaika wa mafunzo hayo na kufanikiwa kuyatekeleza kwa kuripoti habari kwa weledi bila kufanya Ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni.
TAMWA wapaza sauti.
Chama cha Wanahabari Wanawake kimeendelea kuwa mstari wa mbele katika mambo yanayohusu Wanahabari na kuhabarisha umma kwa ujumla kwani Machi 8, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Rose Reuben wakati dunia ikiadhimisha siku ya Wanawake kwa kuangazia ukatili Mtandaoni alisema bado kuna mapengo kadhaa yanayoibua changamoto za usawa wa kijinsia.
Rose aliasa kuwa, “Teknolojia ikiwamo mitandao ya kijamii, itumiwe vyema kuibua madhara ya ukatili wa kijinsia na habari potofu mtandaoni, kuasa juu ya vitendo vya udhalilishaji na zaidi kuonyesha fursa zinazokuja na ukuaji wake kwa nafasi ya wanawake na wasichana katika jamii.”
Aliendlea kusisitiza kwamba ni wakati sahihi wa kuongeza maarifa kwa matumizi ya teknolojia kama nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko ya kijinsia ili kuwe na taifa zenye usawa.
Kwa upande wake naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya The Launch Pad Tanzania, Carol Ndosi ameiomba Wizara kupitia mamlaka husika kuweza kupitia upya sheria ili ziweze kuwapa uhakika zaidi wa usalama mtandaoni wanawake ili kuweza kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya Kidijitali.
Serikali yavunja ukimya
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum nayo ikasema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya tamaduni kandamizi kwa wanawake na jitihada mbalimbali zinaendelea ikiwemo mapitio ya Sheria ili kuondokana na sheria kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike kwa kuhakikisha wanapata haki na kulindwa.
Hapa Waziri mwenye dhamana ya Wizara hiyo, Dkt. Dorothy Gwajima akakuliwa akisema, “Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali kupitia Wizara yenye dhamana ya masuala ya jinsia kwa Kuendelea kuanzisha na kuimarishwa kwa Madawati ya Jinsia na Watoto katika Vituo vya Polisi ambapo hadi sasa tunayo madawati 420 katika vituo vya polisi.”
Aliyasema haya alipomuwakilisha Waziri Mkuu katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani siku hiyo ya Machi 8, 2023 ambapo ikabainika kwamba kuwepo kwa madawati ya vituo vya polisi kutasaidia iwapo mwanamke akiwa amefanyiwa ukatili kuwa na sehemu ya kushtaki kabla ya kwenda mahakamani.
Wizara ya Habari wafunguka
Wizara ya Habari, mawasiliano na teknolojia ya habari ikiwa kama Wizara ya mama inayohusiana na masuala ya teknolojia haikukaa nyuma katika suala hili la Ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni. Kwa kupitia Nape Nnauye ambaye alikuwa ndiye Waziri mwenye dhamana wa wakati huo.
Akiwa katika Kongamano la Wanawake wa Kitanzania katika TEHAMA lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), Machi 7, 2023, jijini Dar es Salaam alisema, “Waathirika wakubwa wa ukatili mtandaoni ni wanawake na ndio mana kama Serikali tuna wajibu wa kuchukua hatua kali dhidi ya vitendo hivyo”
Nape alitoa rai kwa watu wanaotumia mtandao kusisitiza kuacha kufanya mambo ambayo yasiyotakiwa katika jamii ili kuepuka madhara yanaweza kutokana na matumizi mabaya ya mtandao na kuwapongeza wanawake kwa kuwa makini kwenye ufanyaji wa shughuli zao,na kuwahamasisha kuendelea kushiriki kwa kiwango kikubwa katika TEHAMA ili mapinduzi makubwa ya kiuchumi yapatikane katika jamii zetu.
Nini kifanyike
Katika kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni ni muhimu kuongezeka wingi na juhudi kwa Taasisi za Serikali na zisizo za kiserikali ili kuhakikisha ukatili dhidi ya Wanawake Mtandaoni unaondoshwa ndani ya Tanzania.
Aidha pamoja na mapambano hayo kuendelea ni muhimu pia Taasisi hizo kuwapatia jamii elimu inayohusiana na ukatili Mtandaoni na kuhakikisha kila mwanajamii ana kuwa sehemu ya kumuelimisha mwenzie ili kuondoa ukatili wa Mtandaoni dhidi ya wanawake ili kila mmoja kuwa balozi wa kupinga ukatili huo.
Hitimisho
Utafiti uliowahi kufanywa na taasisi ya Women at Web kwa kushirikiana na TAMWA, ulibaini kuwa, asilimia 79 ya Wanawake wanasiasa na wanaharakati wa kisiasa, walifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa njia ya mtandao wakati wa uchaguzi Mkuu wa 2020.
Ripoti hiyo ilionesha kuwa, uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulikuwa ni moja ya nyakati ambapo idadi kubwa ya Wanawake katika siasa walikabiliwa na unyanyasaji wa mtandaoni, hasa wale wa nafasi za viti maalum 19 vya upinzani ambao walipewa majina na kudhalilishwa mtandaoni kwa muda mrefu.
Hivyo, Teknolojia ikiwamo mitandao ya kijamii, inatakiwa kutumika vyema kuibua madhara ya ukatili wa kijinsia na habari potofu mtandaoni, kuasa juu ya vitendo vya udhalilishaji na zaidi kuonyesha fursa zinazokuja na ukuaji wake kwa nafasi ya wanawake na wasichana katika jamii.
Binafsi ninaamini katika nguvu chanya ya teknolojia na ninatamani Wanawake na Wasichana waitumie kwa ubunifu, ili waweze kujikomboa kijamii, kiuchuni na kisiasa.