Waganga Wakuu wa Mikoa wanaounda kanda ya Nyanda za Juu Kusini, wamekutana katika mkutano wa pamoja na watendaji wa sekta ya afya, ili kujadiliana namna bora ya utekelezaji wa masuala mbalimbali ya uboreshaji wa utoaji wa huduma za fya.
Kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Waziri wa Nchi OR – TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa aliyoyatoa agosti 31, 2024 akielekeza viongozi kufanya mikutano na watumishi inayojielekeza katika utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakabili katika maeneo yao.
Miongoni mwa masuala yaliyogusiwa katika kikao kazi hicho kilichoratibiwa kwa ushirikiano wa Waganga Wakuu wanne wa mikoa Dkt. Ibrahim Isack wa Rukwa, Dkt. Boniface Kasululu wa Songwe, Dkt. Eliza Nyema wa Mbeya na Dkt. Jonathan Budenu wa Katavi Pamoja ni uwajibikaji na usimamizi wa utolewaji wa huduma za afya katika maeneo yao.
Pia kimewajumuisha waganga wakuu wa Halmashauri, makatibu wa afya wa mikoa na halmashauri, wahasibu wa afya na waratibu wa UKIMWI wa mikoa na halmashauri kutoka katika mikoa minne inayounda kanda hiyo ambayo ni Songwe, Rukwa,Mbeya na Katavi.