Takriban Watu 12 wamefariki dunia na wengine 36 kujeruhiwa kufuatia ajali ya basi la AN lenye namba za usajili T282 CXT lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Mkoani Tabora.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoani Mbeya, Wilbert Siwa amesema jali hiyo, imetokea majira ya asubuhi hii leo Septemba 6, 2024 katika eneo la Lwanjiro lililopo Wilaya ya Mbeya vijijini na kuthibitisha kuwa majeruhi walipelekwa Hospitali na kusema atatoa taarifa zaidi.
Akihojiwa na Wanahabari, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Dkt. Darson Andrew amesema amepokea majeruhi hao na kudai kuwa waliofariki ni Wanaume watano na Wanawake saba, huku majeruhi ambao hali zao ni mbaya wakipewa rufaa kwenda Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema, “basi liliacha njia kwenye kona yenye mteremko mkali na kugonga gema na kupinduka na kusababisha vifo vya Watu 12 (Wanaume watano, Wanawake 7) miongoni mwao Watoto wadogo wawili, na kusababisha majeruhi zaidi ya 36 na wenye hali mbaya ni watano.”