Wafanyakazi wa Kampuni maarufu na kongwe Nchini ya DataVision International, wameibua shangwe la ushindi baada ya wote kuvalishwa medali na kupata zawadi mbalimbali, kufuatia kumaliza kwa kishindo mbio fupi na ndefu za Maendeleo Bank Marathon walizoshiriki.
Tukio hilo la hii leo Septemba 8, 2024, limeongozwa na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa jijini Dar es salaam, likilenga kuchangia watoto waliozaliwa njiti katika Hospitali ya KCMC ya Mkoani Kilimanjaro na ujenzi wa kituo cha kulelea Watoto yatima cha Dikonia, kitakachojengwa Wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani.
Washiriki kutoka taasisi mbalimbali za ndani na nje ya Mkoa wa Dar es salaam pia walifanikiwa kumaliza mbio hizo za Kilomita 2.5, Kilometa 5, Kilometa 10 na mbio ndefu za Kilometa 21, hali ambayo ilionesha mwitikio chanya wa zoezi hilo.
Baadhi ya Wafanyakazi wa DataVision International waliohojiwa na Dar24 Media wamesema, mbali na ukimbiaji uliowapa ushindi, pia wamepata hamasa ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara, kwani yanaongeza utimamu wa mwili, ufanisi kazini na kuepuka magonjwa nyemelezi.
Aidha, wakati wa zoezi la ugawaji zawadi mbalimbali na Medali, pia Waziri Mkuu aliunga mkono juhudi za uchangiaji kwa kutoa shilingi milioni 140 zitakazotumika kwa wahitaji waliolazwa KCMC kwa kutoa hundi ya Shilingi milioni 80, huku ujenzi wa kituo cha Dikonia Bagamoyo wakikabidhiwa hundi ya shilingi milioni 60.
Mkoa wa Arusha ndiyo ulioongoza kwa kuwa na wakimbiaji wengi waliojinyakulia zawadi mbalimbali, ukifuatiwa na Dar es salaam iliyowakilishwa vyema na wakimbiaji mahiri wa DataVision International, kisha Mwanza na Njombe.