Takribani Watu 13 wamefariki dunia na miili yao kuteketea kwa moto, huku wengine 45 wakiwemo watoto 19 wakijeruhiwa baada ya kutokea kwa ajali ya barabarani iliyohusisha basi la abiria kugongana na Lori la mafuta, nchini Ivory Coast.
Taarifa ya Polisi wa eneo hilo la Barabara kuu ya A3 inayounganisha miji mikubwa ya Bouake na Korhogo iliyopo kaskazini mwa nchi hiyo imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa 7 usiku wa kuamkia Septemba 7, 2024 huku majeruhi wakiwahishwa Hospitali katika miji ya Katiola na Niakara.
“Hii ni ajali hii mbaya na ilitokea baada ya basi la abiria kugongana na Lori lililobeba mafuta ambalo lilikuwa likitokea upande mwingine, barabara ilikiwa imefungwa na Lori la mizigo, lilikuwa limoegeshwa bila alama yoyote na kupelekea kushika moto,” ilisema taarifa ya jukwaa la tahadhari ambalo hurekodi matukio ya ajali nchini humo.
Nchi nyingi za Afrika, ajali mbaya hutokea mara kwa mara nchini kutokana na ubovu wa miundombinu ya baadhi ya barabara na magari mengi pamoja na utovu wa nidhamu wa madereva ambao hawafuati sheria za usalama barabarani.