Jeshi la Polisi Nchini, limetoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za kweli na za uhakika za mauaji ya kusikitisha ya aliyekuwa kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Ally Mohamed Kibao kuziwasilisha kwa mujibu wa taratibu, ili kusaidia kukamilika mapema kwa uchunguzi wa tukio hilo.
Taarifa ya Msemaji wa Jeshi la Polisi, Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime iliyotolewa Septemba 8, 2024 imeeleza kuwa tayari timu ya uchunguzi wa matukio makubwa toka Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Makao Makuu imetumwa kuongeza nguvu kwenye timu ya awali, ili kuhakikisha waliofanya mauaji haya wanakamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Amesema, wanaendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji hayo ya Ally Kibao ambaye Septemba 7, 2024 aliripotiwa kushushwa kwenye basi la Tashrif na kuchukuliwa na watu ambao hawakuweza kutambuliwa.
“Baada ya kutolewa taarifa za kuonekana mwili wa mtu mwanaume ambaye hakuweza kutambuliwa kwa wakati huo ni mwili wa nani huko Ununio Jijini Dar es Salaam, utambulizi umefanyika kwa mujibu wa taratibu na kubainika ni mwili wa Ally Mohamed Kibao.” ilieleza taarifa hiyo.