Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi wamekutana na kuzungumza na Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Fedha ya Korea kwa ajili ya Ujenzi (K-FINCO), Dkt. Lee Eun Jae pamoja na Watendaji wakuu wa Makampuni Makubwa ya Ujenzi zaidi ya 30 ya Korea Kusini, leo Septemba 9, 2024 jijini Seoul, Korea Kusini.

Katika Mazungumzo yaliyofanyika katika nyakati tofauti, Waziri Bashungwa amewasilisha Mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kuwezesha Makandarasi Wazawa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo ameyakaribisha Makampuni ya Korea kufika nchini na kushiriki katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja na ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.

Ametoa wito kwa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya K-FINCO kuyawezesha Makampuni ya Ujenzi ya Korea kushirikiana na Makandarasi Wazawa katika utekelezaji wa miradi ya ujenzi nchini Tanzania ambayo yatawezesha Makandarasi Wazawa kujengewa uwezo na kupata ujuzi wa teknologia za ujenzi wa miundombinu.

Aidha, Bashungwa ameeleza fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania katika sekta ya miundombinu ikiwa ni pamoja na Korea kushirikiana na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu ya barabara za expressway nq kutekeleza miradi ya kupunguza msongamano katika majiji ya Tanzania wa kwa utaratibu wa PPP, na kuunganisha mtandao barabara na nchi za EAC na SADC.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Fedha ya Korea kwa ajili ya Ujenzi (K-FINCO), Dkt. Lee Eun Jae ameeleza kuwa Serikali ya Korea itaendelea kushirikiana na Tanzania ambapo tayari wameshafanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na kusaini hati za makubaliano na Wizara ya Ujenzi na Taasisi mbalimbali ikiwemo Benki ya NMB.

Mawaziri hao, wakiwa na mwenyeji wao, Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura wanaendelea na ziara ya kikazi nchini Korea Kusini ambapo pamoja na mambo mengine watashiriki Mkutano wa Kimataifa wa Ushirikiano wa Miundombinu kati ya Afrika na Jamhuri ya Korea (Global Infastructure Cooperation Conference – GICC 2024).

Balozi Simuli aridhishwa kazi ujenzi Bomba la Mafuta
Babati: Mpendu awaita Wananchi kujiandikisha, kuboresha taarifa