Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, Freeman Mbowe amesema haitawezekana Jeshi la Polisi kujichunguza lenyewe, huku akimtaka Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni kumshauri Rais kuunda tume ya kijaji itakayoshughulikia uchunguzi wa matukio ya utekaji na mauaji.
Kauli hiyo ameitoa hii leo Jumatatu Septemba 9, 2024 mkoani Tanga wakati akitoa salamu kwenye msiba wa Kada wa chama hicho, Ali Kibao aliyeuawa na kutupwa eneo la ununio jijini Dar es Salaam na watu wasiojulikana.
Amesema, “wote tumesikia kauli ya Rais jana, lakini kauli ya Rais ambayo inaelekeza vyombo vilevile ambavyo ndiyo watuhumiwa namba moja wakajichunguze wenyewe, tunaona hilo haliwezekani, hii nchi haitarekebika.”
Mbowe ameongeza kuwa, Masauni kama mwakilishi wa Rais katika msiba huo anatakiwa kumwambia Rais, rai ya waombolezaji kuwa ni yeye pekee mwenye mamlaka ya kuunda tume ya kijaji ya Kimahakama ambayo inaweza kuchunguza matukio hayo na ambayo yamejificha.
“Leo mnaweza mkaona amani hii inayumba katika msiba huu, kuna siku amani hii msipoangalia itayumba katika mitaa yote ya nchi hii, kwahiyo sisi tunapokasirika ni kielelezo cha tatizo,” alisema Mbowe.