Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo amewataka Watanzania kulinda bunifu zao kwa kuzisajili kisheria, ili zisichukuliwe na watu wengine kutokana na uwepo wa kazi nyingi zinazobuniwa pasipo kufuata utaratibu wa kuzisajili.

Dkt. Jafo ametoa wito huo hii leo Septemba 9, 2024 wakati wa ziara yake aliyoifanya ofisi za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni –  BRELA, jijini Dar es Salaam iliyolenga kujionea utendaji kazi na kujifunza namna Wakala inavyotoa huduma za Sajili mbalimbali.

Amesema, “nawaomba Watanzania mnapokuwa na bunifu zenu mje BRELA kuzisajili maana taasisi hii inakazi ya kulinda haki zenu, na itahakikisha inasimamia majukumu ya kimsingi katika kulinda haki za wabunifu katika nchi yetu.”

Dkt. Jafo ameongeza kuwa, Tanzania imesaini mikataba na nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika – SADC na Soko Huru la Biashara Afrika – AfCFTA, qmbapo Watanzania wanashiriki biashara mbalimbali hivyo usajili wa bunifu zao utasaidia kuwapa haki na kuwalinda kisheria.

Aidha, amewaelekeza watumishi wa BRELA kuwa wawezeshaji wa Wafanyabiashara kwa kuwasaidia kurasimisha biashara zao na si kuwa kikwazo, na kwamba watumie kanuni na sheria kusonga mbele na kama kuna ambazo zina mapungufu ziwasilishwe, ili ziweze kufanyiwa maboresho.

Naye. Prof Neema Mori Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa BRELA wamedhamiria kuhakikisha mazingira ya ufanyaji biashara nchini yanakuwa bora zaidi, kwa kuwawezesha, kuwarahisishia na kutoa usaidizi wa karibu kwa Wafanyabiashara wanaorasimisha, kutoa elimu kwa kuwahusisha wadau mbalimbali.

Awali, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa amesema kwa sasa sera ya miliki ubunifu iko mbioni kupitishwa na baadae kuwa na sheria itakayosaidia ongezeko kubwa la maombi ya ulinzi wa bunifu hizo, ingawa bado kuna jitihada zinaendelea katika kuhakikisha bunifu kuanzia ngazi ya shule ya za msingi hadi Vyuo vikuu, zinalindwa kisheria.

Mbali na jukumu la kusajili miliki, ubunifu na utoaji hati, BRELA pia inatoa ufadhili wa shahada ya uzamili ya miliki ubunifu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa watu watano kila mwaka, ambapo elimu hiyo itasaidia kukuza sekta ya miliki bunifu nchini.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 10, 2024
Daftari la Wapiga Kura: DC Kaganda, Viongozi wa Dini wateta