Huduma za afya mkoani Mwanza zinaelezwa kuboreka katika kipindi cha miezi miwili kufuatia ziara za kushutukiza za wasimamizi wa sekta ya afya ngazi ya mkoa, zinazo ambatana na ushauri wa maboresho ya huduma katika hospitali za halmashauri na vituo vya kutolea huduma za afya mkoani humo.

Kwa mujibu wa Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza, Balandya Elikana, maboresho yanayo shuhudiwa katika kipindi hiki ni mabadiliko makubwa ambayo mkoa uliyatamani kwa muda mrefu na umeanza kuyaona kuanzia mwezi Julai mwaka 2024, ukiyahesabu kama matokeo chanya ya ziara za usiku na za kushutukiza katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za afya ya msingi.

Kauli ya katibu tawala Elikana inafatia ziara yake ya kushutukiza usiku katika kituo cha Afya Igoma kilichopo wilayani Nyamagani jijini Mwanza usiku wa kuamkia septemba 9, 2024 alipofika kukagua na kujiridhisha na mwenendo wa utolewaji wa huduma za afya nyakati za usiku katika kituo hicho ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kukagua mienendo ya vituo vya kutolea huduma za afya mkoani Mwanza.

“Utolewaji wa huduma bora kama hivi mnavyo endelea ndiyo iliyokuwa ndoto ya mkoa, tunataka watu wetu wahudumiwe vizuri muda wote, yaani usiku na mchana tena kwenye mazingira masafi, kwa lugha zenye ufariji na ustaha na ndoto hii imeanza kutimia katika kipindi cha miezi miwili iliyopita, nikupongeze sana mganga mkuu wa Mkoa bila shaka haya ni matokeo chanya ya ziara zako wewe na wataalam wako ambazo mmekuwa mkizifanya katika maeneo mbalimbali ya mkoa wetu,” alisema Elikana.

Katika ziara hiyo, Elikana amekagua maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ikiwa ni pamoja na eneo la wagonjwa wa nje OPD, wodi ya wazazi na sehemu ya kutolea dawa, kadhalika aliongea na wagonjwa ili kujiridhisha na huduma wanazopatiwa ambapo wote walipongeza ufanisi wa madaktari na wahudumu wakieleza kupokelewa kwa ukarimu na kuhudumiwa kwa wakati.

Awali Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba amewaambia waandishi wa habari kuwa kipaumbele cha ofisi yake kwa sasa ni ukaguzi wa miundombinu ya afya katika maeneo ya kutolea huduma za afya pamoja na kutoa ushauri wa kitaalam kwa watumishi walioko chini yake juu ya namna bora ya kuboresha utolewaji wa huduma bora za afya katika ngazi zote za utolewaji wa afya ya msingi ambazo ni Zahanati, Vituo vya Afya na Hospitali za Halmashauri.

Wananchi zikataeni imani za kishirikina - Makalla
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 10, 2024