Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema kuwa dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye maeneo yao.

Kapinga amesema hayo Wilayani Mtwara wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyolenga kukagua visima vya kuzalisha Gesi Asilia katika eneo la Mnazi Bay pamoja na miradi inayofanyika kwa manufaa ya jamii kutokana na uwepo wa gesi hiyo (CSR) ikiwemo ujenzi wa kituo cha Afya na kituo cha Polisi katika eneo la Msimbati.

“Yote haya mnayoyaona ni matunda ya kazi nzuri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anaonesha kwa vitendo jinsi anavyowajali kwa kuhakikikisha mnapata huduma bora kupitia miradi hii,” alisisitiza Kapinga.

Amesema lengo la ziara hiyo ya Kamati ya Bunge ni kujionea thamani ya miradi hiyo ambayo itanufaisha wananchi wa Msimbati, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko aliyoyatoa mara baada ya kutembelea eneo hilo na kuzungumza na wananchi.

Amesema ujenzi wa kituo cha Afya unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Septemba, 2024 huku ujenzi wa Kituo cha Polisi nao ukiwa ukingoni.

Mafuriko yauwa 341, UN yatoa tahadhari
Bermuda Triangle: Sehemu hatari zaidi Duniani