Ofisi ya Umoja wa Mataifa – UN, imesema tangu kuanza kwa mwezi Julai, mafuriko makubwa ya wiki kadhaa nchini Chad yamesababisha vifo vya watu 341 na wengine milioni 1.5 kuathirika.
Ofisi hiyo ya kuratibu misaada ya kibinadamu – OCHA, ilisema majimbo 23 ya nchi hiyo yalikumbwa na mafuriko huku takwimu za Serikali ya Chad zikidai kuwa nyumba 164,000 zimeharibiwa, Ng’ombe 70,000 kufa na ekari 640,000 za mashamba kuharibiwa.
Hata hivyo, Serikali ya Chad bado haijatangaza takwimu rasmi za uharibifu uliosababishwa na mafuriko ambayo yamelikumba taifa hilo lenye watu milioni 16.
Hivi karibuni, Wanafunzi 14 na Mwalimu wao walifariki wakati basi lao lilipoanguka baada ya mvua kubwa kunyesha katika jimbo la Ouaddai katika eneo la mashariki.
Aidha, hadi kufikia katikati mwa mwezi Agosti tayari watu 54 walikuwa wamepoteza maisha kwa mafuriko, huko jimbo la Tibesti, lililopo jangwa la Chad.