Chumvi huwa haifanani na Viungo vingine vya chakula na wala haina harufu inayovutia, lakini bila chumvi nadhani huwezi kula ukafurahia mlo wako.
Wanaume wanaojitambua hawapiganii Nafasi, au Mwonekano bali hupigania kazi inayoleta matokeo hawataki kabisa propaganda wala hawahitaji kuupiga kelele ili wasikike, bali hutambulika matokeo yao.
Chumvi hudumisha uadilifu wake bila kelele, na nina hakika hujawahi kuona ama kusikia mnunuzi wa Chumvi anataka kuionja kabla ya kuinunua, kwa sababu yenyewe tayari imethibitisha ubora wake tangu enzi na enzi.
Ikiwa utahitaji kuapa kwanza kabla ya Watu kukuamini, hapo umekosa kuaminiwa na pengine huna ubora.
Je! Maisha yako katika jamii ni kama Chumvi au ndiyo mpaka uape uaminiwe?
Njia rahisi na pekee ya Chumvi kupoteza ladha yake ni pale inapochanganyika na kitu chochote.
Kwa hiyo angalia na uwe makini na watu wasio na maadili ya kiungwana kwani Chumvi ni ya thamani sana na haipaswi kupotea bure hivyo dumu katika uadilifu.
Dumisha heshima yako
Iwapo siku moja, sote tutaruhusiwa kuweka matatizo yetu kwenye meza na kuyabadilisha, nina hakika kwamba baada ya dakika chache, kila mtu angechukua ya kwake kimya kimya na kuondoka.
Hakuna ukamilifu katika maisha, lakini pia hakuna mtu aliye navyo vyote kwa pamoja yaani ni kweli tuna mapungufu lakini yawe yale tu ya kibinadamu, dumisha heshima yako.
Kama vile nyuso zetu zinavyotofautiana, ndivyo matatizo yetu pia yalivyo, hivyo tunapoingia katika maisha ya wengine basi tubadilishe ladha wajihisi kuna kitu muhimu kimeongezeka kama ifanyavyo chumvi.
Kamwe tusiwe na wivu kwa kile mtu mwingine anacho maana hatujui bei waliyolipa ili kupata walivyonavyo na bei wanayolipa ili kuvitunza.
Ingawa mara nyingi wengi wetu tunatamani kuwa kama watu wengine, basi wao pia wanatamani kuwa kama wewe ulivyo kwa kitu kingine na hawayataki maisha yao maana siri ya maisha ni kama ya mtungi, anayeijua ni kata.
Ridhika jinsi ulivyo na thamini ulichonacho kwani ukiweza yote yawezikana na unaweza kuwa chochote unachotaka, hivyo kuwa na shukrani.