Boniface Gideon, Tanga.
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira imefanya ziara ya kukagua miradi ya Maji inayodhaminiwa Hati Fungani ya Kijani, iliyozinduliwa Februari 22, 2024 na Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ukisimamiwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jijini Tanga – TANGA UWASA.
Hati Fungani hiyo ililenga kukusanya Sh.53.12 ili kutekereza miradi mikubwa ya maji ambapo baada ya kukamilika TANGA UWASA itakuwa na uwezo wakuzalisha lita Milioni 60 kwa siku ikilinganisha na Sasa uzalishaji ni wastani wa lita Milioni 45 kwa siku.
Kamati hiyo, ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jackson Kiswaga ilikagua chanzo cha maji Mabayani ambacho ni kikubwa kinachotegemewa kwa kutoa huduma jiji la Tanga na mtambo wa kutibu na kusambaza maji, Mowe.
Kiswaga alisema lengo la ukaguzi huo ni kuona namna fedha zilizotolewa na serikali zinavyotumika katika kutekeleza miradi ya maji.
“Wananchi tuwape maji na utekelezaji wa mradi wa hatifungani uanze haraka ili kutimiza azma ya Rais ya Kumtua mama ndoo ya maji kichwani,” alisisitiza Kiswaga.
Aliipongeza Wizara ya Maji na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tanga, TANGA UWASA kwa kazi wanayoifanya katika kuwapeleka huduma ya Maji Wananchi, ili kuondosha tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Tanga.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema maji yatakayozalishwa kupitia mradi wa hati fungani utaweza kuhudumia na maeneo ya jirani hivyo jukumu la Wizara ya Maji ni kusimamia kuanza kwa mradi huo ukamilike kwa wakati uliopangwa.
“Kwa niaba ya Wizara ya Maji,tunatoa shukrani nyingi sana kwa kamati hii, kitendo cha kukagua miradi mikubwa kama hii na kuridhishwa ni jambo kubwa na lakujivunia, niwaahidi wajumbe wa kamati hii na wakazi wa Mkoa wa Tanga, kuwa tutaendelea na mapambano ya kumtua mama ndoo kichwani inatimia kabla ya 2025,” aliongeza Aweso.