Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha kunakuwa na unafuu katika upatikanaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ikiwemo mitungi ya gesi ili kumwezesha kila mwananchi kutumia nishati iliyo safi na salama.
Dkt. Biteko amesema hayo Septemba 13, 2024 jijini Dodoma wakati wa hafla ya Kusainiwa mikataba ya ushirikiano ya utekelezaji wa Nishati Safi ya Kupikia yenye thamani ya shilingi bilioni 50.98 kati ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na taasisi sita ambazo ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Jeshi la Magereza (TPS) na Wasambazaji wa Gesi ya kupikia, hafla ambayo ilienda sambamba na uzinduzi wa jengo la REA.
Amesema, katika kutekeleza jitihada hizo, Serikali imetoa ruzuku kwa mitungi ya gesi zaidi ya 400,000 itakayouzwa kwa nusu gharama ya awali ambayo inasambazwa katika mikoa yote Tanzania Bara huku zoezi hilo likiwa ni endelevu.
Kuhusu mikataba hiyo ya Nishati Safi ya Kupikia, Dkt.Biteko ameiagiza REA na wadau kuhakikisha kuwa matokeo yanaonekana tena kwa uharaka akieleza kuwa “itakuwa aibu sana watanzania wanaona mikataba imesainiwa huku kukiwa hakuna matokeo, tusione kawaida kwa ndugu zetu kupoteza maisha kwa kutumia nishati isiyo safi, tuwaokoe kupitia miradi hii na tutumie kila fursa inayojitokeza.”
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ameagiza Watendaji wa Wizara ya Nishati kuhakikisha kuwa majengo ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake yanafungwa mfumo wa umeme jua ikiwa ni kuonesha kwa vitendo matumizi ya nishati safi yenye gharama nafuu.
kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema tukio hilo ni alama ya ushirikiano kati ya REA na Taasisi za Jeshi ambapo amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za dhati katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, udhibiti wa rasilimali za misitu na kutengeneza fursa za ajira kupitia Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema kwa sasa nishati inayotumika kupikia chakula cha Wafungwa na Mahabusu ni kuni kwa asilimia 98 ambapo Jeshi hilo lilianza kutekeleza Mkakati wa Nishati Safi ya Kupikia kwa kuanza kutumia nishati safi kupitia gesi asilia na mkaa mbadala hivyo kusainiwa kwa mkataba huo kutawezesha Jeshi la Magereza kutumia nishati safi ya kupikia kwenye magereza yake.
Amesema kuwa Wizara ya Mambo ya Ndani itahakikisha fedha zilizotengwa pamoja vifaa kwenye programu hiyo zinasimamiwa ipasavyo ili lengo tarajiwa lifikiwe na hii ikienda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watumishi wa Jeshi ili waweze kuisimamia na kutunza miundombinu itakayofungwa.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy alisema kuwa, Wakala huo kuhamia kwenye jengo lake kumewezesha kuokoa shilingi milioni 650 zilizokuwa zikitumika kwa mwaka kulipia kodi ya pango ambazo sasa zinaelekezwa kwenye maendeleo ya huduma zinazotolewa.
Kuhusu mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia alisema kwa upande wa Jeshi la Magereza, mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 35.23 ambapo kati ya fedha hizo 75.5% ambayo ni sawa na shilingi bilioni 26.57 zitatolewa na REA na 24.6% sawa na shilingi bilioni 8.66 zitatolewa na Jeshi hilo kwa mradi utakaotekelezwa kwa muda wa miaka mitatu katika Magereza 129 ya Tanzania Bara.
Mkataba wa Magereza unahusisha masuala mbalimbali ikiwemo ujenzi wa mifumo ya bayogesi (gesi vunde) 126, usimikaji wa mifumo 64 ya gesi ya LPG, usimikaji wa mfumo wa gesi asilia, usambazaji wa mitungi ya gesi (LPG) ya kilo 15 ikiwa na jiko la sahani mbili ipatayo 15,920 kwa watumishi wa Magereza na usambazaji wa tani 865 za mkaa mbadala unaotokana na makaa ya mawe kutoka STAMICO.
Mhandisi saidy alisema kwa upande wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) mikataba iliyosainiwa ina thamani ya shilingi bilioni 5.75 ambapo kati ya fedha hizo asilimia 76 ambayo ni sawa na shilingi bilioni 4.37 itatolewa na REA na huku asilimia 24 sawa na shilingi bilioni 1.39 itatolewa na JKT.
Alisema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika Kambi 22 za JKT kwa muda wa miaka miwili itakayohusisha ujenzi wa mitambo 9 ya bayogesi, majiko 291 ya kutumia mkaa mbadala (makaa ya mawe na tungamotaka), ujenzi wa mifumo 180 ya kupikia inayotumia LPG na sufuria zake, ununuzi wa tani 110 za mkaa unaotokana na makaa ya mawe, ununuzi wa mashine 60 za kutengeneza mkaa mbadala na mafunzo kwa vijana wapatao 50,000.
Wadau wengine waliosaini mikataba ya Nishati Safi ya Kupikia ni kampuni zinazofanya biashara ya gesi ya mitungi ikiwemo Taifa Gas, Manjis, Oryx pamoja na Lake Oil ambapo wanasambaza mitungi ya gesi ya kupikia ipatayo 452,445 kwa bei ya ruzuku katika mikoa yote ya Tanzania Bara.