Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezindua huduma saba ikiwemo maabara maalumu (skills lab) itakayowajengea ujuzi wahudumu wa Afya Kanda ya Kati na mikoa ya jirani, pia amepongeza watumishi wa Hospitali kwa kutoa huduma bora za afya.
Uzinduzi huo, umefanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa – BMH, ukilenga kuimarisha huduma za afya, huku pia akizindua vyumba maalumu vya upasuaji vinavyotembea (mobile theatre truck) kuwawezesha wataalamu kufanya upasuaji nje ya BMH.
Huduma ya tatu iliyozinduliwa na Mhagama ni pamoja na kituo cha huduma kwa mteja (Call Centre) kwa BMH, ili kurahisisha mawasiliano kati ya BMH na wateja wake.
Huduma nyingine aliyozindua ni vyumba vipya vya upasuaji vitatu hivyo kufikisha vyumba 11 na hivyo kuongeza wigo wa huduma ya upasuaji kwa BMH.
Waziri Mhagama pia amezindua Miongozo ya Matibabu (SOPs), Huduma kwa Wateja wa BMH, Miongozo ya Idara ya Kutoa Huduma, Kujiendesha na Kujenga uendelevu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali, Prof Abel Makubi, amesema watumishi wa Hospitali wameshirikishwa katika kuandaa Standard Operating Procedures (SPOs).
“Niwasifu sana watumishi wangu wa BMH wameshiriki kikamilifu katika kuandaa SPOs ambazo zitatuongoza katika kutoa huduma,” Amesema Makubi.
Akitoa neno la shukrani, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Dkt. Deodatus Mtasiwa, amesema kuanzishwa kwa Hospitali ya Benjamin Mkapa ni kutokana na muhtasari wa Hospitali kama saba za India, hivyo ndiyo tukaja na BMH.
“Hata mchoraji wa Hospitali hii ni mtanzania baada ya kuangalia muhatasari wa Hospitali saba za India,” amesema Dkt. Mtasiwa.