Serikali imesema kuwa nishati ya umeme ni nguzo muhimu katika maendeleo ya kiuchumi ya Taifa na kuwa inachochea shughuli za uzalishaji viwandani, huduma na kuboresha maisha ya wananchi. Na ni matarajio ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona umeme wa uhakika unafika kwa kila Mtanzania ili kuimarisha maendeleo na kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko jijini Dar es salaam wakati akizinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Amesema, “Ni muhimu kuendelea kusimamia utekelezaji wa miradi mingine ya kimkakati, ikiwemo ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji, mfano mradi wa Malagarasi mkoani Kigoma na miradi mingine ya uzalishaji iliyopo katika hatua za utekelezaji. Pia, kuhakikisha tunaendeleza vyema vyanzo mseto vya umeme ikiwemo mathalani mradi wa umeme wa jua Kishapu mkoani Shinyanga na uendelezaji wa nishati ya jotoardhi nchini,’’ alisema.

Aidha, Dkt. Biteko ameipongeza Bodi hiyo mpya ya TANESCO kwa kuhakikisha Watanzania wanapata umeme wa uhakika na kuitaka kuongeza jitihada za kuimarisha huduma kwa wateja huku akiwataka kutojihusisha na vitendo vya udalali katika zabuni zitakazotangazwa na Shirika.

Amesema, “Watanzania wanataka wapate umeme wa uhakika na walipe kama walivyotumia, wanataka nishati safi ya kupikia. Sisi Wizarani tumejiwekea kipimo cha kupimana kila robo mwaka tunakutana na kuangalia utekelezaji wa kila taasisi na nyie Bodi sasa wapimeni watu wenu.’’

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba amesema kuwepo kwa Bodi hiyo mpya malalamiko kuhusu TANESCO yamepungua na hiyo ni ishara ya kusimamia vizuri Shirika.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Dkt. Rhimo Simeon Nyansaho amesema kuwa Bodi imekuwa ikipata ushirikiano mzuri kutoka Wizarani sambamba na kupata wajumbe wa Bodi wenye sifa, vigezo na utaalamu kutoka katika nyanja mbalimbali.

Aidha, Dkt. Nyansaho amesema wameendelea kushirikiana na Wizara kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo ya upatikanaji wa umeme ambayo kwa sasa imepungua na hivyo wamejikita katika usambazaji wa umeme.

Akizungumzia kuhusu kuwezeshwa kwa wakandarasi wa wazawa ili waweze kushiriki katika miradi ya TANESCO, Dkt. Nyansaho amesema ni vizuri Wakandarasi wazawa wapewe uzito kwenye manunuzi kwani kuna uwezekano asilimia kubwa ya fedha inaenda nje ya nchi.

Dkt. Biteko aliteua Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) yenye wajumbe nane Machi 18, 2024.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 17, 2024
Sheikh Mkuu: Waislam tuache vitendo viovu, tudumishe amani