Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya amesema Rais Dkt Samia Suluhu Hassan tayari imetoa zaidi ya shilingi Bilioni 830 kwa ajili ya kujenga upya na kwa ubora zaidi barabara na madaraja yalioathiriwa na mvua za El -Nino na kimbunga Hidaya nchini kote .
Amesema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami inayojengwa na mkandarasi M/s China Railway Seventh Group (CRSG), na kuhimiza umuhimu wa ujenzi huo kuwiana na thamani ya fedha na kukamilika kwa wakati ili wananchi wanufaike na mradi huo mapema iwezekanavyo.
Alisema, “tunakwenda kujenga pale palipokuwa karavati la mita mbili tutaweka daraja la mita tano, daraja lenye upana wa mita 20 tutajenga mita 40 baada ya kujifunza kwamba hayamaji yanaweza kuja kwa kiasi kikubwa sana. Watanzania naomba walielewe hilo kwamba kote kulikokuwa kumekatika tunakwenda kujenga upya na kwa ubora zaidi ili turudishe miundombinu ya barabara zetu katika ubora wake.”
Kasekenya amesisitiza umakini na kasi katika ujenzi wa daraja la Mbambe lenye urefu wa mita 81 linalounganisha mji wa Ikwiriri na Mkongo pamoja na barabara ya Nyamwage – Utete (Km 33.7) kwa kiwango cha lami ili zikamilike haraka na kuchochea shughuli za usafiri na usafirishaji wilayani Rufiji.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo amewahakikishia wakazi wa Kilwa, mkoani Lindi kuwa barabara ya Tingi-Kipatimu itajengwa kwa lami kwa awamu huku madaraja katika barabara hiyo ujenzi wake unatarajiwa kuanza mapema mwezi Oktoba, 2024.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Brabara (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Mhandisi Baraka Mwambage amesema ujenzi wa barabara hiyo una jumla ya makalvati 109 ambapo kati ya hayo mawili yamekamilka na ujenzi wa kalvati moja unaendelea.
Naibu Waziri Kasekenya anaendelea na ziara yake katika Mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara na madaraja hususan yalioathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.