Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema utekelezaji wa Falsafa ya 4R unaotanguliza Utaifa na Utanzania kwa kiasi kikubwa umeweza kuliunganisha Taifa na kuepusha migawanyiko na tofauti za kisiasa na kiitikadi.

Rais Dkt. Samia amesema katika kudumisha amani na usalama wa nchi, Serikali inasimamia utekelezaji wa Falsafa ya 4R sambamba na kusimamia kikamilifu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sheria za nchi kupitia Jeshi la Polisi.

Rais Dkt. Samia amesema hayo wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Maafisa Wakuu Waandamizi wa Jeshi la Polisi Tanzania na Maadhimisho ya Miaka 60 ya Jeshi la Polisi uliofanyika katika Chuo cha Polisi.

Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa utekelezaji wa Falsafa ya 4R umeimarisha uhuru wa vyama vya siasa, uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa raia kwa ujumla, na kuwaleta watu pamoja katika kujenga nchi. Aidha, amesema Serikali itahakikisha mafanikio hayo hayarudishwi nyuma.

Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Samia amerejea kuwa Jeshi la Polisi litachunguza visa vya upotevu wa maisha, na wahusika kuchukuliwa hatua na amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi ili kukomesha matukio hayo yanayopingwa na wananchi wote.

Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kusimamia ipasavyo maadili ya askari ili Jeshi litoe huduma stahiki na kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi hilo.

Miongoni mwa masuala ambayo amelitaka Jeshi liyafuatilie ni pamoja na uhalifu wa aina mbalimbali unaofanywa kupitia mitandao.

Kuelekea chaguzi za Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, Rais Dkt. Samia amelitaka Jeshi la Polisi kuimarisha usalama katika kipindi chote cha kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Waagizwa kubainisha Watoto wenye mahitaji maalum
Wapanga kuuwa Tembo 200 wagawe nyama kwa Wananchi