Boniface Gideon – Tanga.

Serikali imeweka bayana makosa ya kuepuka wakati wa mchakato wa kushiriki zoezi la kupigaji kura, uchaguzi Serikali za mitaa, huku ikitahadharisha wenye tabia ya kujiandikisha kwenye kituo zaidi ya kimoja na watakaotoa taarifa za uongo kuhusu uraia wao watawajibishwa.

Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi Dkt. Batilda Buriani wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusema yapo makosa kadhaa yatakayomtia hatiani mwananchi au mjumbe yeyote anayegombea katika uchaguzi huo.

Amesema mtu yeyote atakuwa ametenda kosa la uchaguzi, endapo ataharibu orodha ya wapiga kura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi pamojana kutishia wapiga kura au wagombea, ili kuvuruga uchaguzi na kufanya kampeni siku ya uchaguzi atakuwa anakiuka utaratibu.

Mkuu wa mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Burian akizungumza na waandishi wa Habari.

Dkt. Batilda pia amesema kosa jingine ni kuonesha ishara na kuvaa mavazi yanayo mtambulisha mgombea au chama cha siasa, mita 200 kutoka kwenye kituo cha kupigia kura pamoja na kumzuia msimamizi wa uchaguzi au wa kituo, atakayeteuliwa kutekeleza majukumu yake, kukiuka masharti ya kiapo chake, kupatikana kwa karatasi ya kupigia kura zaidi ya moja kwa nafasi moja.

“Makosa yapo kadhaa ikiwemo la mjumbe au mwananchi yeyote,atakaye bainika kuvuruga au kuvunja ratiba ya mikutano ya kampeni ya uchaguzi, kukutwa na silaha kwenye eneo la uteuzi wa wagombea,” alisema RC Batilda.

Aidha, ameongeza kuwa kutangaza matokeo ya uchaguzi, kabla hayajatangazwa rasmi na msimamizi wa uchaguzi, kufanya jambo lolote kinyume cha kanuni ya uchaguzi pamoja na sheria nyingine za nchi zinazohusiana na uchaguzi hayatafumbiwa macho.

“Adhabu ya makosa hayo ni faini isiyozidi laki tatu, kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja. Hivyo ni vizuri wananchi wakajua makosa haya,ili wasije kujikuta kwenye matatizo,” alisema.

Waandishi wa Habari wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dkt. Batilda Buriani.

Aliwataka wananchi kujiandikisha kwenye daftari la mpiga kura ,ifikapo Octoba 11,mwaka huu ili wasipoteze haki ya kuchagua viongozi wanahitajika kwa maendeleo ya Mkoa na maeneo yao.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi mkoani Tanga wameiomba Serikali kuongeza muda wa kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura wakisema siku 10 pekee hazitatosha kwani wengi wanabanwa na muda wa kutekeleza majukumu yao.

“Wakati mwengine yanatokea matatizo mbalimbali katika vituo vya kujianfikishs au kupigia kura.Hivyo suala la huduma ya kwanza ni muhimu,kwani kwenye maeneo hayo wengine ni wazee na wagonjwa,” alisema Mohamedi Dondo, Katibu wa Wazee Asili, Wilaya ya Tanga na kuongeza:

Naye Majid Shali alisema, uchaguzi ni haki ya kila Mtanzania, ingawa kumekuwa na tabia ya vijana wengi kutopiga kura kisha wanalalamikia viongozi hawafai.

“Ili kupata viongozi bora ni lazima tujitokeze na kujua kura ni haki yetu, tunapaswa kujumuika ili kuchagua viongozi bora na siyo kusubiria kuchaguliwa na watu wengine,” aliongeza.

Fountain Gate Royal Fans yazinduliwa Babati
Maisha: Hii hapa Dawa ya migogoro ndani ya ndoa