Boniface Gideon – Tanga.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amepongeza maafisa madini wakazi wa mikoa kwa kuvunja rekodi ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 196 kwa kipindi cha miezi miwili katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi ambacho ni zaidi ya kiasi cha shilingi bilioni 161 kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha 2015/2016.
Waziri Mavunde aliyasema hayo hivi karibuni kwenye kikao kazi na menejimenti ya Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na wakurugenzi, mameneja na maafisa madini wakazi wa mikoa chenye lengo la kuweka mikakati ya kuimarisha Sekta ya Madini katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia ukusanyaji wa maduhuli, udhibiti wa utoroshaji wa madini, udhibiti wa mianya ya upotevu wa makusanyo na kuimarisha usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri sana ya ukusanyaji wa maduhuli hasa katika kipindi za kuanzia mwezi Julai hadi sasa ambapo kiasi cha shilingi bilioni 196 zimekusanywa, kiasi ambacho kinazidi kiasi kilichokusanywa kwa mwaka mzima wa fedha wa mwaka 2015/2016,” alisisitiza Mavunde.
Katika hatua nyingine Waziri Mavunde alisema Serikali imeipa kipaumbele Sekta ya Madini ikiwemo uwekaji wa mazingira rafiki ya uwekezaji na kuongeza bajeti ya Wizara ya Madini kutoka shilingi bilioni 89 hadi shilingi bilioni 231 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025.
“Bajeti hii kubwa tuliyopewa inakwenda kutatua changamoto mbalimbali katika Sekta ya Madini ikiwa ni pamoja na ununuzi wa vifaa kama vile magari 89 na pikipiki 140 ambazo zitatumika kuyafikia maeneo yote yenye shughuli za uchimbaji wa madini na ukusanyaji wa maduhuli.
Aidha, Mavunde aliwataka maafisa madini wakazi wa mikoa kusimamia Sekta ya Madini kwa kufuata Sheria na kanuni za madini na kusisitiza kuwa wasisite kuchukua hatua za kisheria kwa haki pale sheria na taratibu zinazozimamia Sekta ya Madini zinapokiukwa.
Maagizo mengine ni pamoja na Ofisi ya Kamishna wa Madini kwa kushirikiana na Ofisi za Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa kushirikiana kwa pamoja kuwalea, kuwakuza na kuwaendeleza wachimbaji wadogo wa madini na kuimarisha ushirikiano kati yao na watumishi na watendaji wengine wa Sekta ya Madini.
Wakati huohuo akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amepongeza hatua ya Waziri Mavunde kuendeleza falsafa yake ya kushirikisha maono yake kwa watendaji wa Wizara na Taasisi hali iliyopelekea Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri kwenye uchumi wa nchi.
“Kupitia ushirikishwaji wa maono yako kwa watendaji wa Wizara ya Madini na Taasisi zake, mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa umeendelea kukua ambapo tuna uhakika ifikapo mwaka 2025 utakuwa umefikia asilimia 10,” amesisitiza Dkt. Kiruswa.