Mbunge wa jimbo la Babati mjini, Pauline Gekul ametangaza ujio wa mashindano ya mpira wa miguu yatakayoanzia ngazi ya vijiji na mitaa kwenye jimbo la Babati mjini yaliyopewa jina la ‘Mama Samia na Gekul Cup’.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo tarehe 19 mwezi Septemba 2024 kwenye ukumbi wa CCM Babati mjini wakati wa tukio la kukabidhi jezi kwa timu zote zitakazoshiriki mashindano hayo ya mpira wa miguu, Mbunge Gekul amesema ujio wa mashindano hayo ni sehemu ya kuiunga mkono serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja shirikisho la mpira wa miguu hapa nchini (TFF) kwa juhudi za kuendelea kukuza sekta ya michezo ikiwemo kuukubali uwanja wa Tanzanite Kwaraa kutumika kwenye mashindano ya ligi kuu Tanzania bara


.
Gekul amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa uwanja sasa ni zamu ya kuwapa fursa vijana kuonesha vipaji walivyonavyo ili wapate nafasi ya kusajiliwa na timu za ligi kuu hapa nchini na kupunguza changamoto ya uwepo wa vijana wengi wasiokuwa na ajira lakini pia kupata timu ya mkoa wa Manyara itakayoshiriki ligi kuu.

‘Lengo letu pia na sisi tuwe na timu ambayo inacheza ligi kuu, na tutaifikia kwa kuibua vipaji huko chini ambapo vijana wetu wapo, hivyo sisi chama na serikali pamoja na viongozi wa timu tunakwenda kuanza mashindano haya katika jimbo zima,’ alisema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu Wilaya ya Babati (BDFA), Gerald Mtui amesema wameyapokea vizuri mashindano hayo kwani lengo kubwa ni kuhakikisha vipaji vipya vinapatikana ambavyo vitaandaliwa kwaajili ya kutumia na kufaidika na uwanja wao wa Tanzanite Kwaraa Stadium.

Mashindano ya Mama Samia na Gekul Cup yanataanza kwa timu za mitaa na vijiji kwenye kila kata kuchuana na baadae kupata mshindi kwa kila kata na mwishowe kila kata kuchuna na kupata mshindi wa jumla wa jimbo la Babati mjini.

Wananchi msijichukulie sheria mikononi - Shaka
Maisha: Ndoto zangu zimetimia kwa mtindo huu