Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuwawezesha wananchi kiuchumi, na tayari imefanikiwa kujenga masoko katika Mamlaka zote za Serikali za Mitaa Unguja na Pemba.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa Tamasha la Pili la Fahari ya Zanzibar, lililoandaliwa na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Zanzibar (ZEEA), katika viwanja vya maonesho ya biashara Dimani, Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema kuwa Serikali imeanzisha utaratibu mpya wa kutumia asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa kuweka utaratibu mzuri wa kutoa mikopo kwa makundi maalum maarufu kwa jina la 4.4.2, ikimaanisha asilimia 4 kwa wanawake, asilimia 4 kwa vijana, na asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu.
Rais Mwinyi ameeleza kuwa utekelezaji wa mipango hiyo umeisaidia Serikali kuvuka malengo iliyojiwekea katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020-2025 ya kuzalisha ajira mpya laki tatu kabla ya kukamilika kwa kipindi cha miaka mitano.
Aidha, ametoa wito kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kujiunga na huduma zinazotolewa na ZEEA kwa kushirikiana na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF).
Ameitaka ZSSF kupanga mipango madhubuti itakayowahakikishia wajasiriamali wanaochangia kwenye mfuko huo kupata mafao kwa wakati.