Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka watumishi wa kada ya afya nchini kutoa huduma bora kwa wananchi ili kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Mhe. Rais za kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kujenga miundombinu rafiki na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa.
Mchengerwa ametoa wito huo akiwa wilayani Monduli, wakati akizindua jengo la wagonjwa wa nje katika Hospitali ya Wilaya ya Monduli lililojengwa kwa lengo la kuimarisha na kuboresha mazingira ya utoaji wa huduma kwa wagonjwa wanaohudumiwa kwenye Hospitali hiyo ya Wilaya.
Amesema, Watumishi wa kada ya afya walio kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya nchini wanatakiwa kujipanga kikamilifu ili kutoa huduma bora kwa wananchi ambazo zinazoendana na uwepo wa miundombinu bora na vifaa tiba ambavyo Mhe. Rais amevitoa kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma.
“Nikisikia popote pale mgonjwa, mama mjamzito au mtoto amefariki kwa uzembe, mganga mfawidhi wa mkoa au wilaya husika uandike barua ya kuacha kazi wewe mwenyewe kwani sitosita kuchukua hatua dhidi yako na mtumishi yeyote akakayebainika kusababisha kifo kwa uzembe,” amesisitiza.
Aidha ameongeza kuwa, Rais Samia alipoingia madarakani aliweka msingi imara wa kuwahudumia wagonjwa kwa kutoa fedha ya kununua magari zaidi ya 500 kwa ajili ya usimamizi na utoaji wa huduma ya dhalura kwa wagonjwa hivyo waganga wafawidhi wa mikoa na wilaya walikabidhiwa magari zaidi ya 222 ili wasimamie utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Amesema, kitendo cha Rais Samia kutoa magari hayo kwa waganga wafawidhi ni maelekezo ya kuwataka kutoa huduma nzuri kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwafuata watumishi katika zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya nchini ili kusikiliza kero na changamoto zinazowakabili na kuzitatua kwa lengo la kuwajengea ari na morali ya kuwahudumia wananchi.