Maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam yameonekana kuwa chini ya Vikosi vya usalama, ili kudhibiti maandamano yaliyoratibiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, wanaoishinikiza Serikali kushughulikia matukio ya Watu kupotea na kutekwa.
Maandamano hayo, hata hivyo yalipigwa marufuku na Jeshi la Polisi nchini, ambapo kupitia Msemaji wake Naibu Kamishna wa Polisi, David Misime alitoa onyo kwa Viongozi wa CHADEMA kuacha kuendelea kuwahamasisha Wananchi kushiriki tukio hilo.
Misime alisema, “Jeshi la polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo asitubutu kufanya hivyo kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika.”
Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Septemba 22, 2024 alisisitiza kuwa maandamano hayo yatafanyika kama ilivyopangwa akisema yatakuwa ni ya amani yanayolenga kuomboleza kuuawa na kutekwa kwa Viongozi wao.