Watu 14 wakiwemo Viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA, wamekamatwa na Jeshi la Polisi kanda maalumu ya Dar es Salaam, kwa tuhuma za kukaidi tamko la Jeshi la Polisi la kupanga na kutaka kufanya maandamano ambayo yalipigwa marufuku.
Kauli hiyo imetolewa hii leo Septemba 23, 2024 na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamisha Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Muliro Jumanne wakati akizungumza na Vyombo vya Habari na kuongeza kuwa maandamano hayo yaliyopigwa marufuku yasingekuwa ya amani.
Amesema, “maandamano yale yasingekuwa ya amani kutokana na baadhi ya matamko yaliyotolewa na hivyo yakapewa katazo kimaandishi kwamba hayatakiwi yafanyike. Lakini Viongozi hawa waliendelea kuhamasishana na kuendelea na matamko mengine mbalimbali yenye viashiria ambavyo vilifanya Polisi iendelee na msimamo wake wa kuyakataza.”
Amewataja Viongozi hao wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – CHADEMA waliokamatwa katika maeneo tofauti jijini Dar es Salaam kwa kukaidi tamko hilo kuwa kuwa ni Mwenyekiti, Freeman Mbowe, Makamu Mwenyekiti, Tundu Lissu, Godbless Lema na Peter Lazaro.
Wengine ni Sheikh Omary Faki, Revokatus Mlay, Paul Mosi, Shaban Mabela Kinga, Aboubakar Abeid, Emmanuel Ruben Ntobi, Slyvester Gasper, Lai Peter Bundala, Mary Isaack Nungu na Habib Bakari Salum, ambao amesema wanaendelea na mahojiano yatakayozingatia misingi ya kisheria.