Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, wamekuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa mipango mbalimbali ya Afya ikiwemo wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Malaria, Kudhibiti UKIMWI na wa Maonjwa Yalisiyopewa Kipaumbele.
Kauli hiyo, imebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ona Machangu amesema Jijini Arusha katika Ufunguzi wa Kikao cha Ushirikiano na Wadau wanaotekeleza Afua mbalimbali za Afya , Lishe na Ustawi wa Jamii kinachoratibiwa na Wizara ya Afya, kwa Kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI pamoja na wadau ikiwemo PACT Tanzania kupitia Mradi wa ACHIEVE.
Amesema, “kuwepo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii pamekuwa na mafanikio mengi katika afua za afya. Pamekuwa na mafanikio makubwa sana uwepo wa CHW’s, kwenye Programu mbalimbali za HIV, Malaria, Kifua Kikuu na Programu nyinginezo nyingi.“
Dkt. Machangu amesema Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yatakayoanza tarehe 30, Septemba, 2024 yatasaidia kwa kiwango kikubwa katika kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa upande wake Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Norman Jonas amesema Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii utakuwa na mchango mkubwa kusogeza huduma karibu na mwananchi huku Afisa kutoka Mpango huo Dkt. Meshack Chinyuli akisema mikoa 10 ya kuanzia inatekeleza mpango huo.
Naye Mratibu wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. May Alexander amesema Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii yatafanyika kwa miezi sita ikiwemo miezi mitatu mafunzo nadharia na miezi mitatu mafunzo kwa vitendo.
Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa rasmi Januari 31, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ambapo Septemba 19, 2024 Waziri wa Afya, Jenista Mhagama alitangaza kuwa Mafunzo ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.
Mafunzo hayo, yanatarajiwa kuanza Septemba 30,2024 ambapo jumla ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 11, 515 watapatiwa Mafunzo hayo na dhamira ya Serikali ni kufikia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii 137, 294 katika Mikoa yote ya Tanzania katika kipindi cha miaka mitano katika kufikia dhana ya afya kwa wote ifikapo mwaka 2030.