Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia Afya, Dkt. Festo Dugange amekagua na kuzindua ukarabati wa Miundombinu kisha kufungua Hospitali ya Shunga Misheni iliyopandishwa hadhi kuwa hospitali katika halmashauri ya Wikaya Kasulu mkoani Kigoma Leo Septemba 26, 2024.
Akizungumza mara baada ya kukagua Majengo ya Hospitali hiyo, Dkt. Dugange ambaye amemuwakilisha Waziri Mkuu Kasim Majaliwa kwenye ufunguzi huo, amesema serikali inathamini kwa kiasi kikubwa ushiriki wa taasisi binafsi katika kutoa huduma za Afya hivyo ofisi yake itaendelea kuziunga mkono taasisi hizo ili kuendelea kusogeza huduma za uhakika za kiafya kwa wananchi.
Amewahimiza wakazi mkoani Kigoma na Tanzania kwa ujumla kufika kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya wanapopata maradhi ili kupima na kufahamu sababu za kuugua badala ya kujielekeza kwenye tiba Asili.
Amesema, “Serikali na wadau wa maendeleo wamekuwa wakitumia mabilioni ya fedha kuwekeza kwenye sekta ya Afya, hivyo niwahamasishe nyote kuendelea kutumia na kunufaika na huduma za Afya kuendana na maelekezo ya wataalam wetu.”
Aidha Naibu waziri amezitaka taasisi zisizo za kiserikali zinazotoa huduma za kiafya kuajiri wataalam wenye sifa sambamba na kufanya kazi kwa kuzingatia miongozo ya utoaji wa Huduma za Afya inayotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Ukarabati wa Hospitali hiyo umetekelezwa kwa gharama ya Shilingi Bil.2.4, Fedha kutoka kwa wafadhili Taasisi za kidini Readycharity ya Austria, Alliance Mission pamoja na marafiki wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Magharibi ya Tanganyika Mkoani Kigoma kutoka nchini ujerumani.

Kijiji wanachoishi Wachawi 96 pekee, wana tuzo za mwaka
Maisha: Mpenzi wangu aliyechepuka na Bosi nimemrudisha