Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema ni wakati wa Bara la Afrika kubadilika kwa kutumia Nishati Safi ya Kupikia ili kutoathiri afya na mazingira kutokana na matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na mkaa.

Dkt. Samia ameyasema hayowakati akizindua Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Iliyopo Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma ambayo imefungiwa mifumo ya Nishati Safi ya Kupikia.

“Kilichonifurahisha zaidi nilipofika hapa ni matumizi ya nishati safi ya kupikia, huu ni mradi wangu nilioubeba kwa ajili ya wanawake wa Afrika,” amesema Rais Samia

.Ameongeza kuwa, Wanawake wengi Afrika wamekuwa wakipata maradhi kwa ajili ya matumizi ya nishati zisizo safi kama kuni na hivyo kupoteza maisha.

Amesema hivi sasa Taasisi kubwa ikiwemo za elimu ambazo zina idadi ya zaidi ya watu mia moja Serikali itaanza nazo kwa kuzifungia mifumo ya nishati safi ya kupikia.

Awali, Naibu Waziri Nishati, Judith Kapinga amesema mradi huo wa nishati safi katika shule hiyo umetekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) huku Oryx Gas wakifadhili mtungi mkubwa wa kilo 1,750.

“Hapa watakuwa na uwezo wa kutumia nishati hii kwa mwezi mmoja na nusu hadi miezi miwili, hivi sasa wana wanafunzi takriban 500 lakini majiko haya yanauwezo wa kupikia hadi wanafunzi 800,” amefafanua Kapinga

Ameongeza kuwa, pamoja na kufungwa kwa mifumo hiyo, elimu ya matumizi sahihi ya nishati safi ya kupikia imetolewa shuleni hapo.

Mahundi atimiza ahadi kwa Wafungwa Gereza la Ruanda
Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Septemba 28, 2024