Kiwanda cha kisasa cha East Africa Conveyor Supplies Limited (EACS) kilichopo Kahama, Shinyanga kimeanza rasmi uzalishaji wa vipuri vya mitambo vinavyotumika kwenye migodi na viwanda mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni matokeo ya jitihada za Serikali katika kuweka mazingira bora na wezeshi ya uwekezaji pamoja na Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini.
Akizungumza Mjini Kahama, Mkoani Shinyanga na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini, Mkurugenzi Mtendaji wa EACS, Peter Kumalilwa, alisema kuwa kiwanda hicho kimeanza uzalishaji Mei 2023 na vipuri vinavyozalishwa ni pamoja na steel conveyor frames, drop brackets, steel conveyor rollers, impact conveyor rollers, plastic na steel caps for conveyor rollers.
Amesema, bidhaa hizo zinauzwa kwenye migodi mbalimbali nchini kama Barrick North Mara, Barrick Bulyanhulu na Buckreef, pamoja na migodi iliyo katika nchi jirani kama Kibali Gold Mine uliopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Lumwana Mine uliopo nchini Zambia.
Kumalilwa alibainisha kuwa, malighafi nyingi zinazotumika katika kiwanda hicho, ikiwemo chuma na nondo, zinatoka katika viwanda vya ndani ya Tanzania, hivyo kuchangia katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini, sambamba na kupunguza gharama za uagizaji wa vipuri hivyo kutoka nje ya nchi kwa baadhi ya migodi hapa nchini.
Kuhusu soko la bidhaa hizo, amesema ubora wa bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho umevutia masoko mengi, wakitarajia kupanua biashara zao hadi nchi za Afrika Magharibi na kwamba bidhaa hizo zinatumika katika viwanda vya saruji na viwanja vya ndege.
Aidha, ametoa rai kwa taasisi za kifedha kuwaunga mkono Watanzania ambao wamejikita kwenye uzalishaji wa vipuri au wanapanga kuanzisha viwanda kama EACS kwa kuwapa mikopo yenye riba nafuu na kuongeza kwamba, mikopo hiyo itawezesha Watanzania kushindana na wawekezaji wa nje ambao mara nyingi wana mitaji mikubwa.
Kumalilwa pia amewasisitiza Watanzania kuchangamkia fursa zilizopo katika migodi, badala ya kubaki mijini akisema, “nataka niwasisitize Watanzania kuwa madini ni maisha. Changamkieni hizi fursa. Tuje huku migodini tuangalie fursa gani tunaweza kufanya, hasa kwa kushirikiana na wawekezaji wa nje au kwa asilimia 100 ya Watanzania.”
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Kimadini Kahama, Winnifrida Mrema alisema kuwa uwepo wa Kiwanda hicho ni jambo la kujivunia kwani ni moja kati ya miradi itakayosaidia kuliendeleza eneo la mgodi wa Buzwagi ambao upo kwenye hatua ya kufungwa baada ya shughuli ya uzalishaji wa dhahabu kukoma, hivyo kurahisisha upatikanaji wa vipuri ambavyo awali vilikuwa vikiagizwa kutoka nje ya nchi.
Amesema, kupitia uwepo wa kiwanda hicho, Watanzania watapata fursa ya kujifunza ujuzi kuhusu teknolojia mpya na kubainisha kuwa hatua hiyo ni moja ya uwekezaji mkubwa nchini unaoleta fursa za kiuchumi na ajira kwa Watanzania.
Naye, Meneja wa Ufungaji Mgodi wa Buzwagi Zonnastraal Mumbi alieleza kuwa katika mipango ya ufungaji mgodi huo, moja kati ya hatua za uendelezaji wa eneo hilo ni kuanzishwa kwa Eneo Maalumu la Uwekezaji Kiuchumi (SEZ) ambapo viwanda tofauti vitajengwa.