Wanawake nchini, wamehimizwa kuchangamkia fursa zilizopo katika sekta ya madini, ikiwemo kuwekeza kwenye shughuli za uchimbaji pamoja na kutoa huduma kwani Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa kila mtu kushiriki katika uchumi wa madini bila kujali jinsia yake kwa kuzingatia Sheria.

Wito huo, ulitolewa Mjini Kahama na Mchimbaji Mdogo Asha Msangi maarufu kama Mama Nakio wakati akizungumza na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Madini, walitembelea shughuli za uchimbaji Wilayani Kahama, Shinyanga.

Mama huyo qmbaye pia ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Manda Gold Mine, anamiliki leseni 12 za uchimbaji mdogo wa madini (PML) na alianza safari yake ya kibiashara katika kilimo cha mpunga.

Hata hivyo, amesema kutokana na azma yake ya kufanikiwa zaidi, aliamua kuingia kwenye shughuli za uchimbaji wa madini, hatua ambayo imebadilisha maisha yake.

Amesema, “kwa msaada wa Serikali, niliweza kupata leseni, jambo ambalo limenifungulia milango zaidi kwenye sekta hii ya madini, wanawake wanayo nafasi kubwa katika kuchangia mnyororo wa thamani kwenye sekta hiyo kama ilivyo kwangu.”

Mama Nakio aliongeza kuwa, “Wanawake wanayo nafasi kuanzia uchimbaji hadi usindikaji, ukiangalia hapa wengi ndio wanaoongoza kutoa bei nzuri yaununuzi wa mawe na wanajipatia vipato vinavyokimu maisha na familia zao, wao ndio wanaotoa huduma za vyakula kwenye maeneo ya wachimbaji.”l

 

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Kahama, Winfrida Mrema alieleza ugumu uliokuwepo kwa wanawake kushiriki katika shughuli za uchimbaji wa madini tofauti na kipindi cha sasa kwani Serikali imeweka mazingira wezeshi na rafiki kwa kila mtu kushiriki katika uchumi wa madini bila kujali jinsi yake.

Alimpongeza Mama Nakio kwa juhudi zake, akisema kuwa ni mfano wa kuigwa na kusema “mfano mzuri tunao hapa Kahama, huyo Mama Nakio ameonyesha kuwa inawezekana, amejikita katika sekta hii na sasa anaendelea kufanya vizuri, kwa kweli tunawaomba wanawake wengine wajitokeze kwa wingi na kuchangamkia fursa hizi.”

Sekta ya madini imekuwa ni nguzo muhimu katika uchumi wa Tanzania, na kwa kuhusisha wanawake, inawezekana kuongeza kasi ya ukuaji na maendeleo endelevu. Kupitia ushuhuda wa Mama Nakio ameonyesha kuwa, kwa kujituma na kujiamini, wanawake wanaweza kufikia mafanikio makubwa katika sekta ambazo hapo awali zilionekana kuwa za wanaume pekee.

Aidha, Serikali kupitia Wizara ya Madini iko mbioni kuzindua Programu ya Uchimbaji kwa Kesho Bora (Mining for a Brighter Tomorrow – MBT) yenye lengo la kuwajengea uwezo makundi ya kina mama na vijana.

Makundi hayo ni yale wanaojishughulisha na shughuli za Uchimbaji wa Madini pamoja na mnyororo mzima wa Sekta ya Madini nchini. MBT itawasaidia Wanawake na Vijana kwa kuwaendeleza au kuwainua kwa kuwapatia leseni za maeneo ya kuchimba, magari, vifaa na mitambo ya uchorongaji.

Kweli Dunia imejaa maajabu, Karibu Ziwa Rosa - Retba