Washtakiwa wanne wa kesi ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024, akiwemo Askari Magereza na wa Jeshi la Wananchi – JWTZ, wamehukukiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile Binti Mkazi wa Yombo, Dar es Salaam.
Hukumu hiyo, imetolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na ilikuwa ikiwakabili Washtakiwa hao MT 140105 Clinton Damas maarufu kama Nyundo ambaye ni Askari wa JWTZ, Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson maarufu kama Machuche na Amin Lema (Kindamba).
Katika kesi hiyo ambayo pia ilifahamika kama kesi ya waliotumwa na Afande, upande wa Jamhuri uliwasilisha mashahidi 18 na vielelezo 12, ili kuthibitisha mashtaka dhidi ya Washtakiwa.
Kwa mara ya kwanza Washtakiwa walifikishwa Mahakamani Agosti 19, 2024 na kusomewa mashtaka hayo mawili mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule ambapo walikana mashtaka na kukosa dhamana.