Maadhimisho ya siku ya Wazee duniani hufanyika Oktoba 1 ya kila Mwaka, yakilenga kuelimisha jamii haki na stahili mbalimbali zinazohitajika kwa Wazee hao, sanjari na kuwakumbusha umuhimu wa uwepo wao katika jamii husika.
Waswahili husema ‘Uzee ni dawa’ lakini pamoja na umaarufu wa msemo huo, bado Wazee wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo matibabu, hasa kutokana na kunyemelewa na maradhi mbalimbali yasiyoambukiza.
Wazee ni watu muhimu, ambao wengi wametulea nakutokana na kasi ya maisha na siku kwenda mbio, umri wao sasa umesogea hali inayolazimu Taifa kuwatazama kwa jicho la ziada.
Kutokana na ukweli huu, Serikali inatakiwa kubadili mfumo wa upatikanaji wa huduma ya Wazee uliopo na ijikite katika kuwapatia wazee bima ya Afya ya Daraja la juu kuweza kuwasaidia kiuhakika.
Ikumbukwe kwamba Wazee wengi huchukuliwa kama tabaka lilotengwa, hivyo Serikali katika kuwatunza wasiiishie kutoa huduma za matibabu pekee, bali hata kujua makazi yao, vyakula na kuwasaidia vipato kama ilivyo kwa mataifa mengine.
Siku hii ya Wazee Duniani, ilianzishwa mwaka 1990 baada ya Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ikiwa na lengo la kutambua mchango wao katika jamii na kuhamasisha heshima, haki, na ustawi juu yao.
Kwa mujibu wa takwimu za karibuni, inakadiriwa kuwa hadi kufikia mwaka 2050, karibu asilimia 21 ya watu wote duniani watakuwa ni Wazee, hivyo Vijana wa leo hawana budi kujipanga na kujiandaa kuukabili uzee.