Wanawake Viongozi nchini, wametakiwa kujifunza kuongoza kutoka kwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ambaye ni kielelezo cha Uongozi imara, hodari, makini na madhubuti nchini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Wahitimu wa mafunzo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Wizara ya mambo ya nje, Naomi Zegezege wakati wa kufunga mafunzo ya Uongozi na usimamizi Jumuishi na endelevu kwa wanawake 30 waliyoyapata katika shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha Mkoani Pwani.

Amesema, kozi mbalimbali na Mafunzo yanayotolewa Shuleni hapo ya kuwajengea uwezo wa Uongozi kundi la Wanawake Viongozi ni agizo la Rais Dkt. Samia akilenga Wanawake Viongozi kupata elimu iliyokusudiwa.

Kupitia mafunzo hayo Wanawake Viongozi wamepata tofauti kati ya mtu na Taasisi, kuboresha mahusiano kazini, viongozi na Serikali pamoja na kuwa na Taasisi zenye kufanya kazi kwa ufanisi na bila kusahau kutimiza wajibu wao katika familia kama akina Mama wa familia.

“Mafunzo haya ni sehemu ya Maagizo ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ambayo amekuwa akihimiza Wanawake wapate mafunzo mbalimbali ya kujimarisha katika kazi zao na sisi tunaahidi kwenda kuleta mabadiliko kwenye nafasi zetu,” alisema Zegezege.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazothamini mchango wa mwanamke katika uongozi na ngazi mbalimbali za kiutendaji ndiyo maana Rais Samia amekuwa akitoa maelekezo kwamba ni lazima wanawake wajengewe uwezo, ili waweze kugombea nafasi mbalimbali na kupewa majukumu makubwa ya kuongoza inapobidi.

“Washiriki tumejifunza masuala muhimu ya Uongozi kwa upana kuanzia maeneo muhimu yanayowezesha shughuli za serikali kufanyika bila kuingiliwa kama vile masuala ya Usalama wa Taifa tukianzia na ulinzi wa mipaka, na raia wake, umuhimu wa upatikanaji wa huduma za jamii, pia historia ya ukombozi wa Afrika ili tujue nchi imetoka wapi, iko wapi na inaelekea wapi,” alisema Naomi.

Kwa upande wake Afisa Mkuu rasilimali watu kutoka NMB, Emmanuel Akonay alisema mafunzo hayo yatawasaidia washiriki kutatua vikwazo vinavyowakabili na kuleta matokeo chanya sehemu zao za kazi.

Naye Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Prof. Marcellina Chijoriga alizishukuru Taasisi zilizowaruhusu wafanyakazi wao Wanawake, kushiriki mafunzo hayo huku akiwataka kuwa mabalozi wazuri wa masomo yanayotoleiwa shuleni hapo.

Dkt. Msonde ateta na menejimenti NCC