Faudhia Simba, Dar24 Media – Dar es Salaam.

Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia migawanyiko ya kimawazo kwa vizazi vipya na vile vya zamani juu ya mabadiliko ya kiteknolojia, yanayodhaniwa kuwa yameharibu utamaduni na wengine wakiona yameleta maendeleo.

Lakini kiuhalisia, mambo mengi kwasasa yamebadilika tofauti na zamani ambapo ni wazi inaonekana kuwa kuna utofauti wa kimazingira, kifikra, mitindo ya maisha nk.

Mfano hapo mwanzo ilikuwa ni ngumu sana wazazi kuwaruhusu watoto kukaa na watu ambao wanaona wana mapungufu kimaadili, tofauti na sasa ambapo watu hudhani ni usasa kukaa na wahuni au wavuta bangi ikichukuliwa kama ni ujanja.

Ukimuona mtu anavuta kilevi cha moshi kwasasa sio kitu cha ajabu tena kama hapo awali, lakini pia kundi hilo au makundi hayo yamezidi kuongezeka kiasi kwamba kuna kazi haziwezi fanyika bila kuvuta kilevi cha moshi ama kimiminika.

Mfumo wa fikra wa zamani ulikuwa ukichukulia vitu vigumu ambavyo sasa ni virahisi, mfano wengi waliamini vazi la dera ‘vijora’ ni maalum kwa wadada micharuko (walioshindikana), lakini sasa vazi hilo limekuwa la kawaida kwa kila rika.

Walisema kijora ni nguo ya shughuli na waovaa ni watu waliojitoa ufahamu na ni waswahili, lakini sasa hivi imekuwa tofauti kwani hata baadhi ya ambao walikuwa wakiona hivyo wamekuwa na mtazamo tofauti, maana hata walioamini kuwa wanaopenda shughuli ni wazaramo nao wamekuwa wazaramo.

Kiukweli, mtindo wa maisha umebadilika kwa kiasi kikubwa kwani hata mwanamke aambaye awali alionekana ni kiumbe dhaifu sasa wapo katika maeneo, sekta na hata nafasi nyeti wakiwa na majukumu makubwa ambayo zamani ilikuwa ni nadra kutokea.

Si ajabu kama zamani kwasasa kumkuta mwanamke akiendesha Pikipiki, Basi, Lori, Bajaji au ni fundi Makenika nk, ambapo zamani  ilikuwa ni ajabu na sio rahisi kufanya hivyo, kwani aibu zilitawala, hofu na hata kimaadili au kukosa ruhusa kwa familia au mume.

Mfano Wanaume wengi hawakutaka kuona Wanawake wao wakitafuta kama wao, Mwanamke alichukuliwa ni pambo na chombo cha starehe au mama wa nyumbani mwangalizi wa familia.

Zama zibebadilika kiukweli, sasa si ajabu kuwaona Wanawake wakicheza mpira wa miguu ama kuwa mabondia tena kwa umahiri hasa, michezo ambayo awali hawakuwa wakiipa kipaumbele na ilionekana ni ajabu.

Kuna marais Wanawake si Tanzania pekee hata Liberia imewahi tokea hivyo, ikiwemo Marekani sasa Kamala Harris ambaye ni Makamu wa Rais akiwania nafasi kamili akishindana na Donald Trump, yupo Clara Luvanga ni mcheza soka wa kulipwa huko Uarabuni, mwanadada Opa Clement aliyeko Uturuki akisakata soka pia na wengine wengi.

Mifano ipo mingi lakini pia ni utandawazi huu huu ambao leo umefanya tuone baba akitembea na mjukuu ama mtoto wake katika sehemu za starehe wakiwa nusu uchi kimavazi na inaonekana ni jambo la kawaida ama usasa,  haya yote yamesababishwa na utandawazi.

Utandawazi umefanya dunia kuwa kijiji, umewapa watu ujasiri wa kufanya mambo yasiyofikirika, umefanya watu kuwa na uthubutu wa kujaribu mambo na wakapata matokeo kielimu, kibiashara, kisayansi na hata eneo la Afya, wakipata ufahamu ambao zamani ilikuwa nadra kupatikana kwa urahisi.

Kijiji hiki ambacho kimeletwa na utandawazi, kimeendelea kuleta athari chanya na hasi katika jamii, maana waswahili walisema penye riziki hapakosi fitna, hivyo usemi huu unaakisi kwamba huenda lengo la waanzisha mitandao lilikuwa jema lakini wabaya nao wamepitishia maudhui yasiyofaa eneo hilohilo, ili kuivuruga jamii.

Msemo mwingine ni ule wa kizuri hakikosi kasoro, hivyo kama wana jamii ni vyema wenyewe tukachuja na wasimamia maudhui wakaendelea kuyasimamia kwa weledi ili kama Taifa libaki katika utamaduni wake kwani kiuhalisia kwenye utandawazi kuna mazuri mengi zaidi kuliko hasara ukiitumia vyema.

Milioni 5 za Canal kutatua changamoto Shule ya Tutu 
Mbinu iliyowasaidia wengi kufaulu mitihani ya Chuo